BOIPLUS SPORTS BLOG

MADRID, Hispania
KITENDAWILI cha vigogo gani watapambana katika kuwania taji la ubingwa wa çsoka barani Ulaya, kimepata jibu usiku huu baada ya Real Madrid kuitandika Manchester City bao 1-0 na kuifuata Atletico Madrid iliyotinga hatua hiyo jana baada ya kuiondosha Bayern Munich.

Bao pekee katika mchezo huo lilifungwa na winga wa Wales, Gareth Bale katika dakika ya 20 akimalizia pasi fupi ya mlinzi wa kulia Danny Carvajal.

Baada ya bao hilo timu ziliendelea kushambuliana kwa zamu ingawa Madrid walitawala zaidi mpira hadi kipindi cha kwanza kinaimalizika. Kipindi cha pili Madrid walionekana kuanza kucheza kwa tahadhari kubwa hali iliyopelekea City wafike golini kwao mara nyingi zaidi ingawa mashambulizi yao hayakuzaa matunda.

Hadi mwisho wa mchezo Madrid waliibuka kidedea kwa kuiondoa City kwa jumla ya bao 1-0 kwavile kwenye mchezo wa mwisho timu hizo zilitoka sare tasa.

Kwa matokeo hayo, sasa fainali iliyopangwa kuchezwa Mei 28 itazihusisha timu kutoka jiji la Madrid mchezo utakaochezwa katika dimba la San Siro jijini Milan.

Post a Comment

 
Top