BOIPLUS SPORTS BLOG

LONDON, Uingereza

CHELSEA imeipatia ubingwa Leicester City.....hili ndilo unaloweza kusema baada ya mabingwa hao watetezi 'kukabidhi' kombe kwa wababe wa jiji la Leicester kufuatia sare ya mabao 2-2 waliyoipata dhidi ya Tottenham usiku huu.

Sare hiyo katika uwanja wa Stamford Bridge imeifanya Tottenham ambayo ilikuwa inabanana na Leicester kwenye mbio za Ubingwa ifikishe pointi 70 huku wakibakiwa na mechi mbili ambazo hata wakishinda zote hawatafikisha alama 77 walizonazo mabingwa hao wapya.

Tottenham walipata bao la kwanza katika dakika ya 35 kupitia kwa Harry Kane aliyetumia vema pasi ya Erick Lamela na kumchambua kipa wa Chelsea kabla hajautumbukiza mpira nyavuni.

Dakika 44, Heung-Min Son aliipatia Tottenham bao la pili baada ya kazi nzuri ya Eriksen. Kipindi cha pili Garry Cahill na Eden Hazard waliifungia mabao Chelsea katika dakika za 58 na 83 hivyo kuithibitishia ubingwa Leicester.

Huu ni ubingwa kwanza kwa vijana hawa wa Claudio Ranieri tangu timu hiyo ianzishwe na kwamba sasa wamejipatia nafasi ya moja kwa moja kushiriki michuano ya klabu bingwa barani Ulaya (UEFA).

Post a Comment

 
Top