BOIPLUS SPORTS BLOG

✏Nitike Ahazi
KIUNGO wa zamani wa Simba, Jerry Santo raia wa Kenya ameishauri Simba kutosajili wachezaji wote saba wa kigeni kwani hakuna ulazima huo badala yake watafute wachezaji zaidi wazawa.

Simba imekosa ubingwa kwa miaka minne mfululizo huku wakishindwa kushiriki michuano yoyote ya kimataifa na wametakiwa kuwa makini kuangalia wapi walikosea ikiwemo umakini wa kupokea na kuchambua ushauri wanaopewa kwa sasa.

"Simba ipo kwenye wakati mgumu, hawawezi kujua ushauri mwingine unatoka wapi kwani kwa ukongwe wake si kitu cha kawaida kuendelea kukosa ubingwa miaka minne, lazima wachunguze washauri wao.

"Pia siyo lazima wafikishe idadi ya wachezaji wa kigeni saba, kama wanaweza wasajili straika mmoja makini, kiungo na mabeki ambao watakuwa wanasaidiana na wazawa ila wasifanye sifa kushindana na klabu nyingine," alisema Santo.

Santo ambaye amewahi kuchezea Coastal Union, iliyoshuka daraja msimu huu alionyesha kusikitishwa na kitendo hicho na kuwataka viongozi kuwa makini na soka kwani inasaidia kuwafanya vijana wengi kuepukana na matendo maovu katika jamii.

"Zimeshuka timu zote tatu za jiji la Tanga hiyo ni historia mbaya na aibu viongozi wanaotakiwa kwenye mpira wa miguu wawe wale watu ambao wamecheza soka kwani watakuwa na uchungu na timu, sasa zimeshuka vijana wanaanza kuzagaa mitaani hii ni hatari," alisema.

Post a Comment

 
Top