BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Mbeya
YANGA imemnasa beki wa kulia kutoka Simba, Hassan Kessy ambaye ataleta changamoto kwenye kikosi hicho lakini ujio huo haumtishi Juma Abdul ambaye kwa kipindi hiki amekuwa katika ubora wa juu ingawa ameweka wazi kuwa ushindani utakuwa mkubwa msimu ujao wa ligi.

Akizungumza na BOIPLUS, Abdul alisema kuwa Kessy ni mchezaji mzuri na anajua kukaba, kupiga krosi pamoja na kupandisha timu kutoka upande wa  kulia, kikubwa ni ushirikiano kwa ajili ya kuisaidia timu.

"Namkaribisha kwa moyo mkunjufu, ni mdogo wangu na ninajua ana kipaji kikubwa vile vile atakuwa na mchango mkubwa kwa timu lakini ajue anakuja  kukutana na wachezaji wazuri,'' alisema Abdul.


Beki huyo mwenye uwezo mkubwa wa kupiga mipira iliyokufa alisema timu yao inashiriki michuano ya kimataifa msimu ujao kwahiyo wanahitaji wachezaji wazuri zaidi ya mmoja katika kila nafasi.

Kiwango cha Abdul msimu huu kipo juu kwani amekuwa akicheza vizuri nafasi hiyo na kusaidia kufunga magoli muhimu na moja ya magoli yake yatakayokumbukwa ni bao alilofunga dhidi ya APR ya Rwanda mechi ya ugenini kwa shuti kali la nje ya 18.

Kwa upande wa Kessy nae amekuwa katika ubora msimu huu licha ya kutofautiana na viongozi wake huku akichangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa magoli aliyofunga kinara wa ufungaji wa timu ya Simba Hamisi Kiiza.

Post a Comment

 
Top