BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu,Dar
BEKI wa kulia wa Yanga, Juma Abdul ameteuliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Aprili baada kuwashinda Donald Ngoma  na Hassan Dilunga wa JKT Ruvu.

Katika rekodi za Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB) iliyokaa Jumamosi iliyopita, imeonesha kuwa Abdul alicheza mechi zote tano za Ligi Kuu kwa mwezi Aprili ambapo pia aliifungia timu yake bao katika harakati za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2015/16.

Rekodi hizo pia zinaonyesha kwamba beki huyo hakuonyeshwa kadi hata moja katika michezo hiyo mitano sambamba na kutoa mchango mkubwa katika michezo aliyoshiriki kwa mwezi Aprili.

Abdul atazawadiwa kitita cha Sh.1 milioni na wadhamini wa ligi hiyo Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom.

Uwezo aliouonyesha Abdul ulisababisha Kocha wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ kumjumuisha katika kikosi chake kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Harambee Stars ya Kenya kadhalika Mapharao wa Misri katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika utakaofanyika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam Juni 4.

Wachezaji bora wa miezi minne iliyopita ni kiungo Thaban Kamusoko wa Yanga (Desemba 2015), beki Shomari Kapombe wa Azam (Januari 2016), Mshambuliaji Mohamed Mkopi wa Prisons (Februari 2016) na Shiza Kichuya wa Mtibwa Sugar (Machi 2016).

Post a Comment

 
Top