BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Dar
MJUMBE wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Idd Kajuna ambaye pia alikuwa kwenye Kamati ya Mashindano, Idd Kajuna anakusudia kujiuzuru kufanya shughuli za klabu hiyo.

Kajuna ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja baada ya Simba kupoteza mchezo wake dhidi ya Mwadui kwa kufungwa bao 1-0, mechi iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Tetesi za kujiuzulu kwa mjumbe huyo aliyechaguliwa na wanachama zilianza kusikika tangu jana lakini leo ametamka rasmi kuwa atajiuzulu kutokana na matatizo yake ya kiafya kwani anahitaji kupata muda mwingi wa kushughulikia afya yake.

"Ni kweli nitajiuzulu baada ya kikao, sababu kubwa ni afya yangu, kwasasa sihitaji kuwa na mambo mengi yanayosababisha nitumie nguvu nyingi kuyafikiria," alisema Kajuna ambaye akijiuzulu atabaki kuwa mwanachama wa kawaida tu wa Simba.

Simba imefanya vibaya mechi nne mfululizo, ilifungwa bao 1-0 na Toto Africans ya jijini Mwanza, iliondolewa kwenye michuano ya Kombe la FA dhidi ya Coastal Union kwa bao 2-1, ilitoka sare na Azam FC na kupoteza dhidi ya Mwadui. Wadau wengi wametafsiri kwamba kitendo cha Kajuna kutaka kujiuzulu ni kutokana na matokeo mabaya ambayo Simba wameendelea kuyapata.

Simba inashika nafasi ya tatu kwa kukusanya pointi 58, imeondoka leo asubuhi kwenda Songea ikiwa na wachezaji 13 huku baadhi ya wachezaji wa kigeni wakibaki jijini Dar es Salaam ambapo keshokutwa Jumatano watachezaji na Majimaji.

Post a Comment

 
Top