BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
WACHEZAJI Ibrahim Ajib na Hassani Kessy wametajwa kuwa wasaliti wa timu ya Simba na wamechangia  kwa kiasi kikubwa kuboronga kwa Wekundu hao msimu huu.

Kessy ambaye amesajiliwa na watani wao Yanga alitumia muda mwingi kulumbana na uongozi kushinikiza kulipwa stahiki zake kitu kilichotafsiriwa kama usaliti huku Ajib akicheza rafu ya kizembe na kuoneshwa kadi nyekundu kisha kuondoka kuelekea Afrika Kusini bila kuaga.

Rais wa klabu hiyo Evans Aveva alisema wachezaji hao walikuwa muhimu sana ndani ya kikosi ndiyo maana walirubuniwa na wapinzani wao na kuanza kuwahujumu katika michezo yao.

"Angalia Kessy alisimamishwa na uongozi lakini kabla ligi haijamalizika kasaini Yanga, hii inadhihirisha kabisa kuwa ni msaliti na alikuwa anacheza Simba akili ikiwa upande wa pili, Ajib nae anaoneshwa kadi nyekundu leo, kesho anasafiri kwenda Afrika Kusini hiyo safari aliipangaje kama sio hujuma?" alihoji Aveva.Wakati huo huo Aveva alisema watawachukulia hatua kali za kinidhamu Wachezaji wao watano wa kimataifa waliogomea kusafiri kwenda Songea kucheza na Majimaji kwakua walikiuka makubaliano ya mikataba yao.

"Ni kinyume na makubaliano ya mkataba na walipokuwa wakisaini tuliwaambia, sasa hatua Kali za kinidhamu zitachukuliwa juu yao ili kurudisha nidhamu ndani ya timu," alisema Aveva.

Wachezaji watakaokumbwa na rungu hilo ni Hamis Kiiza, Juuko Murshid, Paul Kiongera, Emery Nimuboma na Brian Majwega.

Katika hatua nyingine Aveva alisema wamejipanga kuwa na kikosi bora chenye wachezaji wenye hadhi ya kuchezea Simba msimu ujao pamoja na benchi kamili la ufundi huku kuhusu suala la ujenzi wa uwanja akiahidi kuwa utaanza punde kwavile tayari nyasi za bandia zimewasili kutoka china.

Post a Comment

 
Top