BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Akram Msangi, Dar
MKONGWE wa soka na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Simba, Hamis Kilomoni amewashangaa viongozi wa klabu hiyo kusajili wachezaji wa kigeni wanaokaa benchi ama jukwaani wakitazama mechi wakati wazawa wanacheza.

Akizungumza na BOIPLUS, Kilomoni ambaye pia ni miongoni mwa wazee wa Baraza la Wadhamini alisema kuwa viongozi wa klabu hiyo wanapaswa kuwa makini kwenye usajili wao hasa wachezaji wageni kwamba wawe ni wale wenye vitu adimu kuvipata kwa wazawa.

''Wanaleta wachezaji ambao hawana hadhi ya kuichezea Simba, mchezaji wa kigeni wa Simba anakaa benchi na imekuwa jambo la kawaida, sioni sababu ya kuleta wachezaji wa aina hiyo wakati hapa wapo, viongozi wanapaswa kuwa makini katika hilo,'' alisema Kilomoni.

Mbali na hilo, Kilomoni alimshauri Rais wa Simba, Evans Aveva kuacha kudharau Baraza la Wadhamini na lile la wazee hao wengi wao ndio walioipigania Simba mpaka hapo ilipo na wao kukuta majengo yamesimama.

''Kauli mbiu ya klabu yetu ni 'Simba nguvu moja' ila inashangaza Aveva ameikumbatia timu hata wanachama hawana nafasi ya kutoa maoni yao, leo hii Simba unaizungumzia ni ya Aveva na kikundi cha watu wachache tu na si vingine,'' alisema Kilomoni.

Simba imesajili wachezaji saba wa kigeni ambapo ni wachache tu wamekuwa wakipata nafasi mara nyingi ya kucheza kama Hamis Kiiza, Juuko Murshid, Emiry Nimubona ambao wapo Dar es Salaam baada ya kugoma kwenda Songea walipokuwa wakidai mishahara yao.

Wengine ni Vincent Angban na Justice Majabvi wapo Songea waliondoka jana baada ya kulipwa mishahara yao huku Raphael Kiongera na Brian Majwega wao hawapati nafasi sana na mara nyingi huwa benchi au jukwaani kama watazamaji na sasa wapo jijini Dar es Salaam.

Post a Comment

 
Top