BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Zainabu Rajabu, Dar
KIUNGO wa Simba Joseph Kimwaga amejiondoa rasmi katika kikosi hicho na kutamka wazi kuwa haitaki tena Simba kwani imempotezea malengo yake.

Kimwaga aliyeenda Simba kwa mkopo akitokea Azam FC ambako alipoteza namba baada ya kukaa nje kwa muda mrefu akiwa majeruhi aliiambia BOIPLUS kuwa timu hiyo imempotezea malengo yake mengi ikiwemo kurudi kwenye kikosi cha timu ya Taifa 'Taifa Stars'.

Mapema mwaka huu tangu Simba iwe mikononi mwa kocha Jackson Mayanja raia wa Uganda alipoteza pia namba hata ya kuanzia benchi hadi pale alipojiondoa kimya kimya ingawa aliwahi kusema kuwa ana ruhusa ya kutatua matatizo ya kifamilia.

“Simba ndiyo walinifuata Azam na kunitaka kwa mkopo kwa sharti la
mimi kucheza ili kulinda kiwango changu kisishuke, viongozi wangu wa Azam walikubali kwa baadhi ya masharti likiwemo hilo la kucheza
kikosi cha kwanza, cha kushangaza hilo sharti wamelivunja.

''Hivyo niliona niondoke zangu na kuwaachia Simba yao huku mimi nikijifua kivyangu na sitarejea tena Simba, nitaangalia maisha kwingine, kikubwa ninataka kwenda kwenye timu nitakayocheza kwa amani bila ya maneno maneno,” alisema Kimwaga.

Tangu ajiunge Simba, Kimwaga ameifungia bao moja katika mechi yao na Stand United iliyochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Post a Comment

 
Top