BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
TIMU ya Azam imepokonywa pointi tatu baada ya kumchezesha beki Erasto Nyoni ambaye alikuwa na kadi tatu za njano katika mchezo namba 156 dhidi ya Mbeya city katika uwanja wa Sokoine ambapo walishindwa magoli 3-0.

Azam wamepokwa pointi hizo kutokana na kukiuka kanuni namba 37(4) ya ligi kuu toleo la mwaka 2015 na kanuni ya 14(37) ya mwaka jana.

Msemaji wa shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF Alfred Lukas ameithibitishia BOIPLUS kuwa  Azam wamepokwa pointi tatu na magoli mawili kutokana na kukiuka kanuni za kumchezesha mchezaji mwenye kadi tatu za njano.

"TFF inawataka timu ya Azam kutunza kumbukumbu za wachezaji wake ili kukwepa adhabu za namna hii," alisema Alfred.

Kwa upande wao Azam kupitia kwa msemaji wake Jaffar Iddi Maganga alisema hawawezi kuzungumza chochote kuhusu hilo kutokana na kutopata barua rasmi toka TFF.

Naye Katibu mkuu wa Mbeya city Emanuel Kimbe ameishukuru TFF kwa kutenda haki na sasa timu hiyo inafikisha alama 33 na kukwepa kushuka daraja hata kama wakifungwa michezo yao iliyosalia ukiwemo dhidi ya Yanga.

Azam ambao walikuwa nafasi ya pili na alama 60 sasa wanabakiwa na pointi 57 wakiwa nyuma ya Simba kwa alama moja huku wakirudi hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi kuu Tanzania bara.

Post a Comment

 
Top