BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
MUDA mfupi baada ya Kamati ya Rufaa ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) kutoa hukumu ya rufani ya upangaji wa matokeo wa Ligi Daraja Kwanza timu za Geita Gold na Polisi Tabora wameipinga hatua hiyo.

Mlezi wa timu za mkoa wa Tabora ambaye pia ni wakili wa timu ya Polisi Tabora, Ismail Aden Rage alisema kamati hiyo imekiuka kanuni za shirikisho hilo huku wajumbe wake wakifanya maamuzi kwa maslahi yao binafsi kitu ambacho atakisimamia hadi mwisho.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kusomwa kwa hukumu hiyo Rage alisema hawakubaliani na hatua hiyo na wanasubiri wapewe ripoti ya maandishi ili wakate rufaa nyingine.

"Sisi Polisi Tabora tumehukumiwa kuhusika kupanga matokeo lakini hawana ushahidi unaoonyesha kuwa tulihusika na kitendo hicho na hiyo hukumu yao ni batili na nitahakikisha haki inapatikana,'' alisisitiza Rage.

Aidha mwenyekiti huyo wa zamani wa klabu ya Simba alisema kesi hiyo bado ni mbichi kabisa na amewahakikishia wana Tabora kuwa haki lazima ipatikane kwa hali yoyote.

Kwa upande wao Geita Gold kupitia mjumbe wa kamati ya utendaji, Sefu Karunde alisema msimamo wao ni kuhakikisha haki inatendeka na kuwazuia wakazi wa mkoa wa Geita kuacha kwenda mahakamani kupinga hukumu hiyo.

Timu ya Mbao FC ya jijini Mwanza imepandishwa kucheza Ligi Kuu msimu ujao kutoka kundi C ambalo Geita ndiye aliyekuwa kinara kutokana na kashfa hizo za upangaji wa matokeo.

Post a Comment

 
Top