BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
TAMASHA la filamu Zanzibar (ZIFF) limetangaza majina ya filamu zitakazoshindanishwa kuanzia Julai 9 hadi 17 visiwani Zanzibar.

Mkurugenzi Mtendaji wa ZIFF Martin Mhando alisema Tamasha lilipokea jumla ya filamu 490 kutoka nchi 32 mwaka huu na kupendekeza filamu 80 zitakazoshindanishwa katika makundi matano maalum.

"Tamasha la mwaka huu litakuwa la kipee kutokana na ubora wa kazi zitakazoshindanishwa huku nchi ya Estonia na Albania zikishiriki kwa mara ya kwanza," alisema Martin.

Aidha Mkurugenzi huyo alisema katika Tamasha la mwaka huu kuna filamu tatu ambazo zitaoneshwa kwa mara ya kwanza duniani ambazo hazijawahi kuonekana mahali popote.

"Mwaka huu filamu za kitanzania zilitumwa 40 na kuchujwa na kubaki 17 huku tano zikishindanishwa katika jopo la Ousmane Sembene.

"Kwa ujumla filamu toka Afrika Mashariki zinazoingia katika mashindano zimeongozeka ambapo kuna nane toka Tanzania, Kenya zipo tano, Uganda tatu na Rwanda mbili."

Washindi watatu wa shindano hili wa mwaka jana walijishindia dola za kimarekani 2,000 kila mmoja kwa ajili ya kuwawezesha kuandaa filamu mpya za kushindanishwa mwaka huu.

Post a Comment

 
Top