BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Mwandishi Wetu, Dar
WAKATI pazia la Ligi Kuu ya Vodacom likitarajiwa kufungwa  Jumapili Mei 22,  kwa timu zote 16 kushuka dimbani, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetoa onyo kali kwa timu zitakazo jiingiza katika mtego wa kupanga matokeo.

Rais wa TFF, Jamal Malinzi ameziasa timu zote kucheza mechi kwa kufuata taratibu, kanuni za ligi kadhalika sheria 17 zinazoongoza mchezo wa soka ambao unapendwa na mamilioni ya watu Tanzania na dunia nzima.

“Nimefanya tathmini yangu na kubaini kwamba, inawezekana kukawa na mipango ya kupanga matokeo. Nichukuwe nafasi hii kuzionya timu zote kutojiingiza huko. TFF iko makini, na ina watu wake kila mkoa ambako michezo hiyo itafanyika, sasa basi naziasa timu kufuata taratibu, kanuni na sheria,” alisema Malinzi.

Mbali ya Malinzi, Bodi ya Ligi nayo imetoa onyo ikisema michezo yote itaanza saa 10.00 jioni hata kama kutakuwa na hali ya mvua katika viwanja husika lengo likiwa ni kukabiliana na upangaji wa matokeo.

Baada ya michezo 29 kwa kila timu, tayari Coastal Union ya Tanga imeaga rasmi ligi msimu huu huku zikisubiriwa timu mbili kwa ajili ya kuungana na Wagosi hao katika kushuka daraja.

Timu ambazo ziko kwenye hatari ya kushuka ni African Sports ya Tanga yenye pointi 26 (nafasi ya 15); Mgambo pia ya Tanga iliyojikusanyia pointi 27 (nafasi ya 14); Kagera Sugar ya Kagera iliyovuna pointi 28 (nafasi ya 13); JKT Ruvu ya Pwani iliyopata pointi 29 (nafasi ya 12) na Toto Africans ya Mwanza yenye pointi 30 (nafasi ya 11).

Kwa hali ya mambo ilivyo, licha ya kwamba Toto inaweza kujihesabu ina nafuu ikilinganishwa na timu nyingine, ukweli unabaki kuwa kwa timu zenye pointi 27 hadi 29 zinaweza kuishusha kama Wanakishamapanda hao watapoteza mchezo wa mwisho au kupata sare huku wapinzani wao wakishinda ambao ni Stand United ya Shinyanga.

Post a Comment

 
Top