BOIPLUS SPORTS BLOG

MILAN, Italia
USIKU wa leo ulimwengu wa soka utasimama kwa muda wa dakika 90, hakuna kingine kitakachokuwa kinaendelea zaidi ya nyasi za dimba la San Siro jijini Milan kukiona cha moto pale miamba miwili ya Jiji la Madrid itakapokuwa inaonyeshana kazi kugombea ubingwa wa Bara la Ulaya.

Ni Real Madrid na Atletico Madrid ambazo zimesafiri umbali wa takribani kilomita 1,162 kutoka Madrid hadi Milan ambako fainali hiyo ya michuano mikubwa na yenye mvuto zaidi duniani (kwa ngazi ya klabu) itapigwa kuanzia majira ya saa 3:45 usiku wa leo.

Timu zilizotinga fainali mwaka huu zinafanana kabisa kwa mengi, lakini hapa nakuletea mambo sita tu.

1. WANAFAMILIA WA LA LIGA
Ligi kuu nchini Hispania 'La Liga' ndiyo ligi inayotajwa kuwa bora zaidi duniani, hili halina ubishi hata kidogo kwavile licha ya timu zake kufanya vizuri kwenye michuano ya Ulaya, pia imekuwa yenye mpira unaovutia zaidi huku ikizalisha vipaji vinavyotamba duniani kote.


Real na Atletico zote zinatoka nchini Hispania huku katika msimu ulioisha timu hizo zimemaliza katika nafasi za pili na tatu kwenye msimamo wa La Liga wakiiacha Barcelona ikitwaa ubingwa. Baada ya fainali ya usiku wa leo hawa wanaweza kupanda ndege moja kurejea nyumbani.

2. WATOTO WA JIJI LA MADRID
Hivi itakuaje siku moja Simba na Yanga za Kariakoo jijini Dar es Salaam zikicheza fainali ya Klabu Bingwa Afrika, halafu mchezo ukapigwe pale Levy Mwanawasa jijini Ndola, Zambia. Heshima ilioje kwa jiji la Dar na Tanzania kwa ujumla.

Tuachane na ndoto hiyo kwavile 'bado ipo ipo sana', na kurejea jijini Madrid ambako kuna hii miamba Real na Atletico. Watoto wa familia moja waalioenda kugombana ugenini, hii ina maana kwa mtindo wowote ule siku ya leo jiji hilo litalipuka kwa shangwe bila kujali nani atabeba kombe.3. WOTE WALIENDA BRAZIL KUTAFUTA MABEKI
Soka la Hispania linatumia zaidi mfumo wa kushambulia kupitia mabeki wa pembeni. Kutokana na hilo, Real na Atletico zote zilifunga safari kwenda nchini Brazil ambako kunasifika kwa kuzalisha mabeki bora wa pembeni.

Real waliwahi kunogewa na huduma ya mbrazil Roberto Carlos, wakaamua kurudi tena na kumchukua Marcelo ambaye amekuwa mhimili mkubwa wa mashambulizi ya timu hiyo. Leo itapambana na Atletico ambayo nayo inaringia beki wa kushoto Filipe Luis kutoka nchini Brazil pia.


4. WALIONGOZANA KUFUATA MABAO UFARANSA
Mpira mabao! Na La Liga ndiyo inayoongoza kwa kutoa washambuliaji wenye mabao mengi zaidi katika ligi kubwa barani Ulaya. Mara kadhaa vigogo wa ligi hiyo wamekuwa wakivuka boda kwenye kusaka washambuliaji.

Real na Atletico zina mastraika kutoka nchini Ufaransa. Karim Benzema amekuwa hatajwi sana kwenye mafanikio ya Real lakini anapokosekana timu hiyo huonyesha wazi kuyumba kwenye safu ya ushambuliaji.Kwa upande wa Atletico wao wanamtegemea Antoine Griezman raia wa Ufaransa ambaye amekuwa tishio kwa safu za ulinzi za timu pinzani kila wakati awapo uwanjani na leo walinzi wa Real wanapaswa kuwa makini sana.

5. WATOTO WA NYUMBANI WAMEPEWA UNAHODHA
Licha ya kukusanya nyota kadhaa kutoka pande zote za dunia, bado timu za Hispania zina kasumba moja kuwa nahodha wa timu akiwa Mhispaniola basi mambo ndio yanakuwa safi.


Raul Gonzalez alimuachia kitambaa Iker Cassilas ambaye alipoondoka klabuni hapo, Sergio Ramos alibebeshwa mikoba hiyo. Wote hao ni wahispania. Atletico wao wanaongozwa na Gabi. Kwa maana hiyo katika fainali ya leo ni lazima Mhispania mmoja atanyanyua 'ndoo' ya UEFA, aidha Ramos au Gabi.

6. NYOTA WAO WA ZAMANI NDIO MAKOCHA
Labda ni kwavile wanaamini kuwa wanazijua vema falsafa za timu hizo, au kwa kuwa walipata mafanikio makubwa wakiwa wachezaji. Lakini mwisho wa siku wao Real na Atletico ndio wanaojua sababu za kuwaajiri wachezaji wao wa zamani kuwa makocha.

Real walimchukua Zinedine Zidane baada ya kustaafu kucheza soka na kumpa majukumu mbalimbali ikiwemo kufundisha timu za vijana pamoja na kuhudumu kama kocha msaidizi chini ya Carlo Ancelot. Baada ya kutimuliwa Rafael Benitez, Zidane alipewa timu na amefanikiwa kuifikisha fainali ya ligi ya mabingwa huku akiukosa ubingwa wa La Liga katika dakika za 'jioni' kabisa.


Kwa upande wa Atletico wao wamefanikiwa kudumu na beki wao wa zamani, Diego Simeone ambaye ameijenga timu hiyo na kuwa ya kiushindani zaidi huku ikizalisha nyota kadhaa wanaogombewa na klabu kubwa barani Ulaya.

Hii inakuwa ni fainali yake ya pili kama kocha wa Atletico huku akiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza dhidi ya Real msimu wa 2013/14. Je, leo mtoto wa nyumbani anapokutana na 'mzawa' wenzake atafanikiwa kulipa kisasi?

Makala hii imeandikwa na Karim Boimanda kwa msaada wa mitandao

Post a Comment

 
Top