BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Mwandishi Wetu, Songea
MATUMAINI ya klabu ya Simba kumaliza ligi kwenye nafasi ya pili yameendelea kufifia baada ya leo hii kulazimishwa sare ya bila kufungana na Majimaji hivyo kushindwa kuwapa faraja wapenzi na wanachama wa timu hiyo.

Huku ikiwakosa nyota wake wengi wa kikosi cha kwanza, Simba ilibanwa mno na Majimaji ambayo ilionekana kukamia kuondoka na pointi zote tatu kwenye mchezo wa leo uliopigwa kwenye dimba la Majimaji mjini Songea.

Hata hivyo timu zote mbili zilionekana kukosa ubunifu na kutumia mipira ya juu ambayo ilikuwa ikiwapa shida washambuliaji wao ambao wengi ni wafupi.

Kocha wa Simba Jackson Mayanja alilazimika kuwajumuisha kikosini wachezaji watatu Mohammed Issah, David Kissu na Hussein Magila kutoka kwenye kikosi cha vijana kutokana na uchache wa wachezaji kwenye kikosi chake.

Hata hivyo ni wachezaji wawili tu wa kigeni ambao wamesafiri na timu hiyo kuja hapa Songea ambao ni Justice Majabvi na Vincent Angban ambao waliwasili jana usiku huku wengine wote wakikosekana kutokana na mgomo.

Baada ya mchezo huo, Mayanja alisema kuwa ameridhika na matokeo hayo na pia amekoshwa na viwango vilivyoonyeshwa na chipukizi aliowapa nafasi.

Sare hiyo imewafanya Simba wafikishe alama 59 huku wakiwa wamebakiwa na kubakia katika nafasi ya tatu.

Post a Comment

 
Top