BOIPLUS SPORTS BLOG

Nitike Ahazi
WAKATI Ramadhan Kichuya wa Mtibwa Sugar akidaiwa kupewa mkataba wa awali wa miaka miwili na Simba, kocha wake Mecky Maxime ameruhusu mchezaji huyo kuondoka na kutamka kwamba haoni tatizo mchezaji wake kuondoka kikosini.

Mecky anaamini kwamba Mtibwa Sugar ni kituo cha kupika wachezaji bora ambao wamekuwa wakigombaniwa na timu kubwa hasa Simba na Yanga hivyo akiondoka Kichuya atatengeneza mwingine.

Akizungumza na BOIPLUS, Mecky alisema kuwa: "Mchezaji anapohitajika na timu nyingine ujuwe kuwa amekuwa bora hivyo sioni tatizo Kichuya kwenda Simba ingawa ana mkataba na sisi wa mwaka mmoja. Viongozi wa Simba wanapaswa kumalizana na viongozi wetu ili tuwaachie."

Akizungumzia juu ya usajili mpya, Mecky alisema "Mtibwa ni kituo cha soka, hatuwezi kuwa na haraka ya kusajili tunasubiri wabomoe kikosi chetu kisha tutasajili majembe mengine yatakayowatikisa msimu ujao kwani sisi tunajua kuibua vipaji vya wachezaji."

Kichuya amewahi kukiri kwamba Simba wanahitaji huduma yake msimu mpya, lakini aliwataka wakamalizane na uongozi wake.

"Ni kweli nimekuwa na mazungumzo nao lakini nina mkataba wa mwaka mmoja, waende wakamalizane na uongozi wangu kwangu soka ni biashara napenda kusonga mbele lakini kwa utaratibu unaotakiwa," alisema Kichuya.

Post a Comment

 
Top