BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Dar
JANA, Shirikisho la Soka nchini (TFF) limeipokonya Azam pointi tatu kwa kumchezesha beki wao Erasto Nyoni mwenye kadi tatu za njano katika mechi ambayo City ilifungwa bao 3-0 na sasa Wapiga Nyundo hao wametamka kuwa TFF waangalie pia malalamiko yao katika mchezo uliovunjika dhidi ya Coastal Union.

Mechi yao na Azam ilichezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya wakati mechi dhidi ya Coastal Union ilipigwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ambapo ilivunjika kutokana na mashabiki wanaosadikiwa kuwa wa Coastal kufanya vurugu zilizopelekea mechi hiyo kuvunjika kipindi cha pili timu hizo zikiwa sare ya ba0 1-1.

Mbeya City ambayo sasa ina pointi 33, ilidai kupelekea malalamiko hayo TFF ambayo bado hajafanyiwa kazi ingawa wamelipongeza shirikisho hilo kufanyia kazi malalamiko yao na Azam huku wakitoa angalizo kwa klabu kongwe kuwa makini kwenye makosa kama hayo.

Mwenyekiti wa Mbeya City, Mussa Mapunda alisema: ''Kwenye hili nawapongeza TFF, hakika wametenda haki, ninawaomba waendelee kusimama kwenye misingi ya haki, ni haki yetu kupata pointi hizo za Azam kwani kumchezesha mchezaji mwenye kadi tatu ni kosa, hata sisi tumekutana na hali hii katika nyakati tofauti lakini hatukuwahi kuthubutu kumchezesha mchezaji mwenye kadi za njani hata kama alikuwa ni muhimu kikosini ila tulimuweka pembeni

''Naamini TFF watatutendea haki hata mechi yetu na Coastal iliyovunjika kutokana na vurugu za mashabiki, mchezo ule ulikuwa na matukio mengi ya ajabu ambayo yalimfanya mwamuzi kushindwa kumaliza mchezo, risasi za moto zilipigwa uwanjani, sisi bado tunasubiri pointi tatu zingine kutoka kwenye mchezo ule," alisema Mapunda

Post a Comment

 
Top