BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Nitike Ahazi, Dar
NAHODHA wa Simba, Mussa Hassan 'Mgosi' ni kama amefika mwisho baada ya kutamka kauli ya kusikitisha huku machozi yakimdondoka timu yake ilipofungwa bao 1-0 na Mwadui.

Mgosi alitamka kuwa ''Tanzania kuna amani laiti kama ingekuwa tupo nchi nyingine, wachezaji wa Simba tungeuwawa," alisema.

Kabla ya kujibu maswali ya mwandishi wetu kuhusiana na mchezo huo uliochezwa uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Mgosi aliinamisha kichwa chini kisha alifuta machozi yaliyokuwa yakimtoka na kuvuta pumzi na kutamka "Wachezaji hawana uchungu na timu."

Mgosi alisema ni wakati wa viongozi hao kuumiza vichwa kusaka wachezaji ambao watatambua ukubwa wa kuvaa jezi hiyo na isiwe ilimradi tu, huku akielezea zaidi kuwa mashabiki wa Simba wameonyesha ustahimilivu na ukomavu wa soka kwani hawajaonyesha vitendo vya kuwazuru.

"Hata tukipita mtaani ni aibu sijui kwa wenzangu wanajisikiaje, tumeitia aibu Simba, nadhani wachezaji hawajitambui na hawajui kwamba Simba ina mamia ya watu," alisema Mgosi

Alisema ni vema wachezaji wakijua kama wameikosea Simba, waombe radhi na kama wataona ni sehemu ya kuchota pesa na kuondoka na wao watapatwa na laana za mashabiki wanaokosa amani.

"Tumewanyima raha mashabiki, jezi tumeifanya haina thamani mtaani inauma siyo Simba ninayoijua ambayo ilikuwa na wachezaji ambao wanajua nini watapaswa kufanya," alisema Mgosi.

Post a Comment

 
Top