BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
KOCHA mpya wa timu ya Azam Zeben Hernandez raia wa Hispania amewasili nchini kwa ajili ya kuchukua mikoba iliyoachwa na Muingereza Stewart Hall.

Azam wamefanya mabadiliko ya benchi lote la ufundi kutokana na kutoridhika na ufanisi wao na kuamua kuwapa mkono wa kwaheri na kumpa kibarua Mhispania huyo.

Mkurugenzi wa mtendaji wa timu hiyo Saad Kawemba ambaye ndiye aliyempokea kocha huyo alisema kuwa watakaa na Mhispania huyo ili wakubaliane kuhusu mkataba huku akitanabaisha mambo yataenda kama yalivyopangwa.

"Kuhusu mkataba tutakaa nae tukubaliane ila ni matumaini yetu kila kitu kitakuwa kitaenda vizuri," alisema Kawemba.Kwa upande wake kocha huyo ambaye ameambatana na msaidizi wake Jonas Garcia alisema lengo lake ni kuifanya Azam kuwa tishio barani Afrika kwa kucheza soka la pasi nyingi kama wanavyocheza FC Barcelona.

Aidha kocha huyo hakusita kuelezea kiwango bora kinachooneshwa na Mtanzania Farid Musa anayefanya majaribio katika timu ya Tenerrife inayoshiriki ligi daraja la pili nchini Hispania na kusema winga huyo anakipaji kikubwa na amefuzu katika timu hiyo.

Kabla ya kujiunga na Azam kocha huyo alikuwa anafundisha timu ya Santa Osua inayoshiriki ligi daraja la pili nchini Hispania.Post a Comment

 
Top