BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
UKIWAZUNGUMZIA viongozi ambao wameongoza Simbana bado wanakumbukwa basi huwezi kuacha kumtaja Sweddy Mkwabi ambaye alipambana na Kaburu pamoja na Jamhuri Kihwelo 'Julio' katika nafasi ya umakamu wa Rais kwenye uchaguzi uliomuweka madakani Rais Evans Aveva.

Mkwabi alizidiwa kwa kura nyingi tu na wapinzani wake Geofrey Nyange 'Kaburu' na Julio, Kaburu ndiye aliyetangazwa kuwa mshindi hata kama Mkwabi au Julio hawakuridhishwa na matokeo hayo ila kura ndizo ziliamua, aliyeshindwa anakubali matokeo tofauti na kwenye siasa ambako mtu anaweza kwenda kupinga mahakamani. Huo ndio uzuri wa soka na maisha yanaendelea kama kawaida kwa maana ukijaribu kwenda mahakamani tu ndio unauaga ulimwengu wa soka.

Baada ya hapo, Mkwabi alijikita zaidi kwenye biashara zake ambazo huzifanyia jijini Tanga ingawa bado ni mwanachama halali wa Simba na ana mapenzi makubwa na timu yake, japokuwa hana nguvu ya kushauri jambo lolote ambalo viongozi wanaweza kulifanyia kazi.

BOIPLUS ilifanya mahojiano na Mkwabi ambaye alikuwa ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji chini ya Mwenyekiti, Aden Rage ambapo alizungumzia mambo mbalimbali katika soka hususani timu yake ya Simba ambayo imekuwa ikifanya vibaya kwa misimu minne sasa tangu wao walipokuwa madarakani.

"Ni kweli Simba ilianza kufanya vibaya kwa kipindi cha miaka miwili tangu tupo madarakani na hii ilitokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya makocha, sikufurahishwa na jambo hilo lakini sikuwa mtu wa mwisho kuamua juu ya hilo na ndiyo sababu kubwa ya kuanza kufeli zikiwemo vurugu za wanachama.

"Tatizo hilo limeendelea hadi sasa ambapo kila kukicha tunabadilisha makocha, hilo ni tatizo maana kila kocha anakuja na mfumo wake ambao kuwabadilisha wachezaji kwa haraka kutoka mfumo huu na kwenda mfumo mwingine si jambo jepesi," alisema. 

USAJILI 
Simba ni timu ambayo inatajwa kutengeneza wachezaji wazuri kutoka kikosi chao cha vijana na pia ni timu inayoongoza kwa kuuza wachezaji nje ya nchi lakini ni timu inayoongoza kutimua wachezaji wakati wa usajili, iwe usajili mkubwa ama dirisha dogo.

"Simba hakuna kawaida ya kuangalia mahitaji ya timu yao linapofika suala la usajili, hakuwi na umakini wanasajili tu kwa kujaza wachezaji bila kujali nafasi ambazo zinapaswa kuongezewa nguvu ama kuimarisha zaidi, ingawa hakuna mchezaji wa bei rahisi kuna wachezaji wazuri na wenye thamani kubwa."TAMBWE, OWINO, MOSOTI 
"Simba walipaswa kumshauri kocha juu ya wachezaji hao, huwezi kumuacha Mfungaji Bora kama Amisi Tambwe, leo hii unawaacha mabeki mahiri kama Donald Mosoti na Joseph Owino na badala yake wameshindwa kuleta mbadala wao.

"Huko ni kukurupuka bila kuzingatia mapendekezo ya wataalamu wa Benchi la Ufundi ambao ndiyo wenye kujua mahitaji ya timu yao, hili ni tatizo ndani ya Simba na mara kadhaa limekuwa likipingwa na kupigiwa kelele.

"Pia wanapaswa kuwa wavumilivu kwa wachezaji wao, hasa mchezaji mpya kama tulivyowavumilia akina Emmanuel Okwi, vinginevyo kila siku kutakuwa na wachezaji wapya na timu itaendelea kufanya vibaya, ukiwa kiongozi unatakiwa kuwa mvumilivu, walipaswa waendelee na malengo yao ya kutengeneza timu na sio kubadilika njiani kutaka ubingwa wakati kikosi bado hakiko imara," alisema Mkwabi

WANACHAMA 
Akili za mashabiki na wanachama zinafanana, kundi hilo huwa linataka mafanikio ya haraka bila kuangalia ubora wa kikosi chao, kimepita katika wakati gani wao huwa wanataka ubingwa tu na ndio jambo la kwanza kwao, Mkwabi amewaeleza kwakusema 

"Wanachama hawana uvumilivu wa muda mrefu, wanachama wanahitaji mafanikio ya haraka ila ikumbukwe kwamba soka ni mchezo wa hatua, Simba wawe na mipango ya muda mrefu, wawe na timu mbili, naamini viongozi waliopo Simba sasa wengi wao ndio waanzilishi wa timu ya vijana, nashangaa na kusikitika kuona wao ndiyo wanaiua timu ya vijana ambayo imezalisha vijana wengi wanaocheza timu ya wakubwa huku wengi waking'aa na timu zingine za ligi kuu."

NIDHAMU 
"Vijana wengi siku hizi wanajitambua, hivyo huwezi kuwaendesha tu jinsi utakavyo, ndani ya Simba wachezaji wengi ni vijana ambao wamewalea wenyewe, wanawapa majukumu makubwa tofauti na umri wao, wanapokosea hawawaonyi kama vijana wadogo wanafoka na kuwakaripia jambo ambalo ni baya sana."Viongozi wa Simba wamewapa usugu wachezaji wao wenyewe, hapo hakuna wa kumlaumu wanashindwa kuishi na wachezaji wao na wanawachukulia kama wote umri wao ni sawa, wamekuwa sugu na hawawezi kuwasikiliza wala kuwaheshimu, kuna lugha za kuzungumza na wachezaji kama hao kulingana na umri wao, naona tayari wachezaji ndani ya Simba wengi wao wameathirika kisaikolojia.

"Kama waliweza kuwavumilia akina Okwi iweje washindwe kuwavumilia wachezaji wao wa hapa, ni jambo la kusikitisha sana, katika uongozi wetu hatukuwa na pesa ila tuliishi vizuri na wachezaji, tuliishi nao kwa mali kauli na mambo yalienda vizuri tu.

"Inasikitisha kuona tunawavumilia wachezaji tusiowafahamu (wa kigeni) wakati wazawa tunawadharau, tunazisaidia nchi za wenzetu kuwa na wachezaji wengi wa kulipwa kuliko kutengeneza wachezaji wetu wengi wa kulipwa ili waisadie Taifa Stars zaidi tunajivunia Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, wachezaji wa kigeni ni sawa wawepo lakini tunaijenga vipi timu ya Taifa," alisema Mkwabi.

AVEVA FUMBA MACHO UANZE UPYA
"Ningekuwa mshauri wa Aveva ningemwambia avunje timu na aitengeneze kwa miaka miwili, hakuna njia ya mkato kwenye soka, jinsi wanavyokwenda wanaonekana waliingia madarakani kwa kukata kiu yao tu. Ujanja ujanja nje ya uwanja umepitwa na wakati, siku hizi timu bora ndiyo inayofanya vizuri hakuna cha mganga wala kuhonga waamuzi, wakiwa na imani hizo hawatafanikiwa kamwe.

"Pia sijaelewa hii Kampuni yao waliyoajiri ya EAG inayodaiwa kushughulikia mambo ya masoko, ni masoko gani wanayoshughulikia ndani ya Simba kwani mpango mkakati uliotengenezwa kwa ajili ya kuiingizia fedha klabu ya Simba umeishia wapi?. Aveva alihusika kwenye mpango huo, kwanini ameuweka kapuni na kuajiri kampuni ambayo naona haina sababu ya kuwepo."Mpango Mkakati uliandaliwa kwa pesa nyingi ukisimamiwa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu Huria (Open Univercity) tulitumia dola 15,000 ambazo alitoa Zacharia Hans Poppe leo hii wanaenda kuanzisha mambo ambayo kuiingizia fedha klabu ni kama ndoto. Aveva anatakiwa kutuliza akili sana kufikiri mambo yake ndani ya Simba," alisema Mkwabi.

UJUAJI NAO TATIZO
"Viongozi wa sasa wote pale Simba wanajuwa kila kitu wala hawawezi kushaurika, kuna mambo mazuri wanayafanya lakini si kwa asilimia kubwa, wanahitajika kubadilika sana ili kwenda na kasi ya mfumo wa soka ulivyo, wakubali ushauri na warudishe umoja ambao kwasasa unaonekana ndani ya Simba hii haupo." 

SPORTS vs COASTAL UNION
Coastal tayari imeshuka daraja, Sports wao bado wanapambana ingawa nao hali yao ni mbaya sana kwani mstari mwekundu umewapitia, ni timu ambazo zipo chini ya Chama cha Soka cha Wilaya ya Tanga kinachoongozwa na Mkwabi, yeye anaelezea mwenendo wa timu hizo.

"Wote hawakuwa na umoja, hawakushirikiana tangu mwanzo, tuliwaita ili kujadili baadhi ya mambo, hizo ni timu za wanachama, mbaya zaidi waliingia katika mfumo wa kubadilisha makocha, sisi kama wilaya kazi yetu ni kushauri tu hatuna lingine zaidi, nguvu kubwa ipo kwenye chama cha mkoa," alimaliza Mkwabi.

Post a Comment

 
Top