BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu
KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa amesema kwamba mchezo ujao dhidi ya Mapharao wa Misri utakuwa ni fainali ya kuamua taifa litakalofuzu katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani kutoka kundi G.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mechi yao ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Harambee Stars uliofanyika jana Uwanja wa Moi Kasarani, Mkwasa alisema kuwa anaamini kwamba Misri wamekuwa wakiwafuatilia kila hatua.

"Najua Misri wanatufuatilia. Na hata Kenya kwa siku zote tatu ilikuwa hivyo hivyo. Najua Misri wanahitaji sare ili wafuzu kwa fainali hizi lakini hawataipata Tanzania," alisema Mkwasa ambaye timu yake itacheza na Misri Jumamosi uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. 

Misri wana pointi saba, Taifa Stars ina pointi moja na hivyo wa kuibania au kupindua matokeo ya Misri isiende AFCON mwakani basi ni Stars hasa kama itawafunga Mapharao hao kabla ya kwenda kucheza na Nigeria Septemba.

"Kama nilivyosema, Misri wanakuja wanahitaji pointi moja. Lakini sisi tunahitaji pointi tatu. Mchezo wa leo unatosha kuona mapungufu (upungufu). Maana ilikuwa mechi ngumu iliyojaa nyota wote wa Kenya ambao ni professionals, lakini mimi nilikuwa na 'local based players' na matokeo yamekuwa hayo.

"Tulianza kufunga bao, lakini wakarudisha. Bora mchezo umeishia hivi maana najua Wakenya hawana uvumilivu, tungewafunga hapa sijui kama tungetoka salama, hawatafanikiwa kwa sababu soka ni mchezo wenye mifumo tofauti. Hivyo tulivyocheza na Kenya sivyo nitakavyocheza na Misri, nitakuwa na mfumo tofauti," alisema na kuongeza.

"Bado tunaendelea kujenga timu yetu, wengi ni vijana kama mlivyoona na wengine ni mara ya kwanza wanacheza. Nimewapa nafasi na mmeona uwezo wao, bila shaka tutafanya vema maana wengine ni U-21 wako kwenye kikosi. Huko mbele tutakuwa na timu nzuri," alisema Mkwasa akimtolea mfano Shiza Ramadhani ambaye alipewa nafasi kwa mara ya kwanza katika kikosi cha kwanza akichukua winga ya kulia.


VICTOR WANYAMA
"Unasema hamkuwa na mchezaji wa kulipwa katika mechi hii, basi mna kikosi kizuri. Wengi ni vijana, wanaweza kama mkicheza kwa kubana kama mlivyotubana hapa, Misri mnaifunga na hata hao Nigeria, si ajabu nikasikia mnakwenda AFCON mwakani. 

Ninaitakia kila la kheri timu hii na Watanzania katika harakati zao. Sisi mwaka huu tumepotea kabisa, hatuna matumaini tena, tunajipanga ndiyo maana nimekuja kutetea taifa langu, hata kama tumekosa nafasi," alisema Wanyama anayekipiga Southampton ya England.

Katika mchezo huo, Taifa Stars iliwakosa nyota wake Mbwana Samatta anayechezea Genk ya Ubelgiji kwa kuwa alikuwa na mchezo muhimu wa kuwania kufuzu fainali za ligi ya Europa ngazi ya klabu Ulaya pamoja na Thomas Ulimwengu anayekipiga TP Mazembe waliokuwa na mchezo mkali dhidi ya AS Vita.

Naye nahodha wa Taifa Stars katika mchezo huo, Mwinyi Kazimoto alisema kwamba mchezo dhidi ya Kenya, umeonyesha picha ya kinachotakiwa kufanyika katika michezo ijayo inayoikabili timu hiyo baada ya kusifu maandalizi, mapokezi mazuri na sapoti kutoka kwa mashabiki wa Kitanzania, hasa wale waliosafiri umbali mrefu kutoka Dar es Salaam kwenda Nairobi, Kenya kuishangilia Stars. 

Post a Comment

 
Top