BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
MATUMAINI ya Simba kuchukua ubingwa msimu huu yamekufa rasmi leo baada ya kukubali kichapo cha goli 1-0 toka kwa Mwadui FC katika mchezo wa ligi kuu Tanzania bara katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku ushindi huo wa Mwadui ukiwafanya Yanga watangaze ubingwa wakiwa na mechi tatu mkononi.

Mechi hiyo ilianza taratibu huku timu zote zikishambuliana kwa zamu na dakika ya tisa almanusura Haji Ugando aipatie Simba goli la kuongoza lakini mpira uliokuwa unaelekea golini uliokolewa na beki Malika Ndeule.

Dakika ya 19 golikipa Shabani Kado alitolewa nje baada ya kugongana na Hamisi Kiiza na nafasi yake ikachukuliwa na Jackson Abdulrazak.

Washambuliaji wa Mwadui Kelvin Sabati na Rashidi Mandawa walikosa nafasi kadhaa kutokana na kukosa umakini huku mabeki wa Simba wakifanya makosa ya mara kwa mara. Simba wao walifanya shambulizi kali langoni mwa Mwadui na kichwa cha mkizi alichopiga Kiiza kilitoka sentimeta chache nje ya lango.

Dakika ya 74 Mwadui walipata goli kupitia kwa Jamali Mnyate baada ya kuwachambua mabeki wa Simba na kupiga shuti la chini nchini lililomshinda golikipa Vincent Agban.

Simba iliwatoa Peter Mwalyanzi, Ugando na Kiiza huku nafasi zao kuchukuliwa na Ibrahim Ajib, Brian Majwega na Musa Hassani Mgosi. Mwadui walimpumzisha Rashidi Mandawa na kumuingiza Julius Mrope.

Dakika ya 90 Ibrahim Ajib alioneshwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu mbaya Hassan Kabunda.

Mwadui imefikisha alama 40 na kubakia nafasi yake ile ile ya sita katika msimamo huku Simba ikishuka hadi nafasi ya tatu na pointi zao 58.

Post a Comment

 
Top