BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
MABINGWA wapya wa ligi kuu Tanzania bara timu ya Yanga wamekabidhiwa kombe la ubingwa baada ya kumalizika kwa mchezo dhidi ya Ndanda ambao walitoka sare ya magoli 2-2 mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mgeni rasmi katika mchezo huo alikuwa Waziri wa Kilimo Ufugaji na Uvuvi Mwigulu Lameck Nchemba ambaye ni shabiki mkubwa wa mabingwa hao waliotetea ubingwa wao baada ya kuunyakua msimu uliopita.

Mechi hiyo ilianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu lakini Ndanda ndiyo walikuwa wa kwanza kupata goli dakika ya 29 kwa mkwaju wa penati lililofungwa na Omari Mponda baada ya Juma Abdul kumchezea madhambi Atupele Green katika eneo la hatari.Iliwachukua Yanga dakika sita pekee kurudisha goli hilo kupitia kwa Simon Msuva baada ya kupokea krosi safi ya Geofrey Mwashiuya upande wa kushoto.

Yanga walipata goli la pili kupitia kwa Donald Ngoma dakika ya 40 baada ya kupokea krosi upande ule ule wa kushoto iliyopigwa na beki Mwinyi Hajji.

Kipindi cha pili Mabingwa Yanga waliendelea kulisakama lango la Ndanda lakini wachezaji wao walikosa ubunifu wanaposogelea lango huku mlinda mlango Jackson Chove akiwa makini muda wote.

Salum Minely aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Burhan Rashidi aliisawazishia Ndanda dakika ya 80 baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na Atupele Green na kumpita mlinda mlango Deogratius Munishi 'Dida'.

Yanga iliwatoa Mwinyi Hajji, Donald Ngoma, Haruna Niyonzima nafasi zilichukuliwa na Oscar Joshua, Matheo Anthony na Mbuyu Twite huku Ndanda ambao ndiyo walikuwa wenyeji wa mchezo waliwapumzisha  Burhan Rashidi, Riphat Hamisi na kuwaingiza Salum Minely,Ahmed Msumi.

Post a Comment

 
Top