BOIPLUS SPORTS BLOG

✏Bakari Kagoma, Dar
MSHAMBULIAJI wa Yanga Paul Nonga ameuandikia barua uongozi wa klabu hiyo umuuze kwa timu nyingine kutokana na kushindwa kupata nafasi katika kikosi cha kwanza.

Katika barua hiyo Nonga ameuomba uongozi huo kumuuza timu nyingine ili kupata nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza kama ilivyokuwa wakati akicheza Mwadui misimu miwili iliyopita.

Rafiki wa karibu wa mshambuliaji huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe katika mtandao huu alisema katika barua hiyo Nonga ameanisha timu ambazo angependa kuchezea msimu ujao huku akikiri mastraika waliopo Yanga wanafanya vizuri kuliko yeye.

Nonga ambaye ana mkataba na Yanga alichukua maamuzi hayo ili kutowatia hasara mabingwa hao wa ligi na kombe la FA ambao walimsajili kwa bei kubwa kutoka Mwadui katika dirisha dogo la mwezi  Novemba mwaka jana.

Kwa upande wake meneja wa klabu hiyo Hafidh Saleh ameiambia BOIPLUS kuwa hajaipata barua hiyo na hajui chochote kuhusu suala hilo.

Nonga ambaye alikuwa moja ya washambuliaji tegemeo kwa timu ya Mwadui alishindwa kufanya vyema ndani ya Yanga baada ya kushindwa katika vita ya namba dhidi ya Amissi Tambwe na Donald Ngoma.

Habari ambazo mtandao huu imezipata ni kwamba kuna uwezekano mkubwa wa straika huyo kurejea Mwadui au Stand United.

Post a Comment

 
Top