BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
PAMOJA na kufanikiwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom  lakini Kocha wa Yanga, Mholanzi Hans van der Pluijm amekiri ugumu wa ligi na kwamba walistahili kutwaa ubingwa huo kwani ana kikosi bora.

Yanga ilitwaa ubingwa na kukabidhiwa kombe lao baada ya mechi yao na Ndanda Fc iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kutoka sare ya bao 2-2 ambapo imefikisha pointi 72 huku wakiwa na mechi moja mkononi dhidi ya Majimaji.

Mholanzi huyo alisema kuwa haikuwa kazi rahisi kutetea ubingwa huo kwakuwa timu nyingi zilijipanga vya kutosha lakini wao walikuwa bora zaidi ndiyo maana waliweza kuunyakua kwa miaka miwili mfululizo.

"Wenzetu walijipanga sana msimu huu  lakini sisi tulistahili kuchukua ubingwa huu kwakuwa tulikuwa na kikosi kipana licha ya kuwa na ratiba ngumu tulicheza mechi nyingi mfululizo mwisho wa siku tulifaulu," alisema Pluijm.

Akizungumzia mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya Segrada Esparanca ya Angola, Pluijm alisema "Katika mpira wa miguu kuna matokeo ya ajabu wakati mwingine tutaenda kwa tahadhari kubwa ili kuweza kulinda ushindi wetu.''

Katika mechi ya awali Yanga ilishinda bao 2-0 ambapo kesho Jumatatu asubuhi wataelekea nchini Angola tayari kwa mtanange huo utakaopigwa Jumatano.

Post a Comment

 
Top