BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu, Dar
RAIS wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino, ameipongeza timu ya soka Yanga kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 2015/16.

Yanga imetwaa ubingwa huo kwa msimu wa pili mfululizo ikiwa ni mara ya 26 tangu kuanza kwa ligi hiyo mwaka 1965.

Katika salamu zake, kupitia barua yake ya Mei 18,  kwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Infantino ameelezea ubingwa wa Yanga kuwa umetokana na kazi kubwa inayofanywa na uongozi wa timu hiyo, makocha, wachezaji pamoja na mashabiki.

“Yanga ndiyo mabingwa wa Tanzania, napenda kuchukua nafasi hii kuipongeza timu nzima kwa mafanikio haya makubwa ambayo ni  matokeo ya mshikamano ulioko ndani ya klabu" alisema Infantino katika barua hiyo na kuongeza

“Kwa niaba ya familia ya soka, napenda kuchukua nafasi hii kuishukuru Yanga na Shirikisho la Soka kwa jinsi mnavyopeleka ujumbe chanya wa soka kwa jamii ya michezo,” alisema Infatino.

Tayari Rais wa TFF, Jamal Malinzi aliipongeza Yanga ambayo imepewa Kombe na medali kwa wachezaji 24, viongozi saba wa benchi la ufundi na viongozi wanne wa Kamati ya Utendaji.


Post a Comment

 
Top