BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
TIMU za Simba na Azam zimeipa nafasi nzuri Yanga ya kutetea ubingwa wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara baada ya kutoka sare ya kutofungana katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo ulianza kwa timu zote kusomana huku dakika ya pili ya mchezo Simba wakipata kona iliyopigiwa na Emery Nimuboma na Hamisi Kiiza kupiga kichwa ambapo mlinda mlango Aishi Manula alipangua na kuwa kona nyingine.

Dakika ya saba kiungo Hamisi Mcha alipata nafasi ambayo angeweza kuipatia goli la kuongoza timu ya Azam baada ya kubaki yeye na mlinda mlango Vincent Agban baada ya beki Juuko Murshid kucheza fyongo.

Mchezo haukuwa wa kasi sana huku viungo wakioneshana umahili katika eneo la kati ya uwanja. Simba walimiliki zaidi lakini walikosa ubunifu walipofika katika eneo la hatari la Azam.

Dakika ya 41 beki David Mwantika alirudisha mpira mfupi kwa mlinda mlango Aishi Manula ambapo Kiiza alichelewa kidogo kuupata kitu ambacho kingesababisha madhara langoni mwa Azam.

Ikiwa imesalia dakika moja timu hizo ziende mapumziko kiungo Peter Mwalyanzi alikosa nafasi ya kuiandikia Simba goli la kuongoza baada ya shuti lake kupaa juu ya goli.

Kipindi cha pili kilianza kwa Azam kumtoa Ramadhani Singano na kumuingiza Mudathir Yahaya na Simba walimuingiza Hija Ugando kuchukua nafasi ya Danny Lyanga aliyepata maumivu.


Baada ya mabadiliko hayo mechi ilianza kuwa na kasi kiasi na kushambuliana kwa zamu huku timu zote zikimiliki mpira kwa zamu lakini walishindwa kutumbukiza mpira kimiani .

Azam walifanya mabadiliko mengine ya kumtoa Kipre Tchetche na kumuingiza Ame Ally 'Zungu' na dakika ya 67 John Bocco almanusura aindikie Azam goli baada ya kupiga mpira kwa mtindo wa kuudokoa lakini mpira huo ukatoka sentimeta chache langoni mwa Simba.

Dakika tatu baadae Bocco tena aliwapiga chenga mabeki wa Simba na kuingia ndani ya eneo la hatari baada ya mabeki wa Simba kushindwa kumkaba na kuachia shuti lililotolewa nje na Vincent Agban.

Simba walifanya mabadiliko ya kumtoa Juuko Murushid na kumuingiza Brian Majwega na Azam kumuingiza Michael Bolou kuchukua nafasi ya Jean Pierre Mugiraneza.

Hadi mwamuzi Methew Akrama toka jijini Mwanza anapuliza kipenga cha mwisho si Simba wala Azam walioweza kupata goli.

Yanga inaendelea kuongoza ikiwa na alama 65 ikifuatiwa na Azam yenye alama 59 huku Simba ikiwa ni ya tatu baada ya kukusanya pointi 58.

Post a Comment

 
Top