BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Dar
LICHA ya Yanga kuhitaji pointi tatu tu ili watangaze ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Wekundu wa Msimbazi Simba hawana habari, walijificha visiwani Zanzibar wakijipanga kushinda mechi zote nne zilizobaki halafu baada ya hapo ndio kieleweke.

Simba wana pointi 58 wakiwa wameachwa kwa pointi 10 na Yanga ambao wenyewe wamebakiwa na michezo mitatu dhidi ya Mbeya City, Ndanda Fc na Majimaji yote wakicheza ugenini.

Endapo Simba watashinda mechi zao zote zilizosalia watafikisha pointi 70  ambazo Yanga wanaweza kuzifikia na kuzipita endapo tu wataifunga Mbeya City na kujinyakulia pointi tatu ambazo zitawafanya wafikishe pointi 71.

Mpira una matokeo ya ajabu ambayo wakati mwingine yanaweza kuustajabisha umma, hii ndio sababu wekundu hao wa Msimbazi hawajakata tamaa ya ubingwa na waliendelea na mazoezi makali walipoweka kambi visiwani Zanzibar ambako huwa wanakwenda pale tu wanapojiandaa na mechi ngumu ingawa leo asbuhi timu hiyo ilitarajia kurejea jijini Dar es Salaam.

Simba ambao kesho Jumapili wataikaribisha Mwadui kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam bado wanaweza kuwa mabingwa endapo tu watashinda mechi zao zote zilizosalia huku wakiwaombea mabaya Yanga wapoteze mechi mbili na kutoka sare mchezo mmoja.

Post a Comment

 
Top