BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
Winga wa Mwadui, Hassan Kabunda

IMEELEZWA kuwa wachezaji watatu ambao walikuwa wanawaniwa na Simba wamepewa mikataba ya awali ili kuwabana wasimwage wino kwenye timu nyingine kwani wanataka waitumikie timu hiyo msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

Wachezaji hao ambao ni beki wa kati Idd Mobi na winga Hassan Kabunda wote wa Mwadui wanadaiwa kusaini mikataba ya miaka miwili kila mmoja huku beki wa kulia kutoka Coastal Union, Hamad Juma naye alitarajia kusaini leo Alhamis.

Mchakato huo umefanywa baada ya kocha wa Simba Jackson Mayanja kupeleka taarifa ya utendaji wake wa kazi ikiwa ni pamoja na majina aliyopendekeza kusajiliwa dirisha litakapofunguliwa pamoja na wale watakaokatwa.

Chanzo cha habari kutoka Simba kinasema kuwa Kabunda yeye bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Mwadui lakini Mobi na Juma mikataba yao imemalizika.

"Wamepewa mikataba ya awali ila huyu Kabunda ndio kuna tatizo kwani hajamaliza mkataba na timu yake. Tutakachokifanya ni kuzungumza na kocha wake Jamhuri Kihwelo 'Julio' ili amwachie nasi tumpe mkataba wa ajira," alisema kiongozi huyo.

Katibu Mkuu wa Mwadui, Ramadhan Kilao aliiambia BOIPLUS kuwa: "Siwezi kumzuia mchezaji kuondoka kama kweli Simba wana nia na Kabunda waje tuzungumze sisi tuna wachezaji wengi ambao hawajaonekana popote.

"Tatizo timu za Dar es Salaam wanasubiri kutengenezewa halafu wawagombanie. Nasema hivyo kwasababu Kabunda amekuwa akisumbuliwa kwenye simu na timu nyingi tu, wakija na tukikubaliana tutamruhusu tu ila Mobi yeye mkataba wake umemalizika," alisema Kilao.

Kilao alisema kuwa kumpa mkataba wa awali hakumaanishi kwamba wamefanikiwa kama hawataenda kumalizana nao kwa kufuata taratibu za usajili kwani mchezaji huyo ana mkataba wa mwaka mmoja mbele baada ya kuongezewa.

Post a Comment

 
Top