BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
SIMBA imemalizana na beki wao wa zamani Donald Mosoti ambapo imemlipa pesa yake yote zaidi ya Sh 64 milioni aliyokuwa akiidai klabu hiyo kwa kuvunja mkataba wake mwaka juzi.

Hivi karibuni Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) liliiagiza Simba kumlipa beki huyo raia wa Kenya na kutoa siku 30 ambazo zingemalizika keshokutwa Jumapili vingenevyo wangeshushwa daraja na TFF ingefutiwa uanachama kwa kushindwa kusimamia suala hilo.

FIFA iliitaka Simba ilipe gharama zote kuanzia pesa ya kuvunja mkataba, faini,fidia pamoja na fedha ya kumlipa mwanasheria wa Mosoti ambazo zote zimelipwa na sasa wapo huru na hawatashushwa daraja.


Mosoti aliithibitishia BOIPLUS kuwa pesa yake imeingizwa Jumanne ya wiki hii ingawa inaonyesha viongozi wa Simba walifanya taratibu za kuingiza pesa hiyo kwenye akaunti yake tangu Mei 19.

"Nashukuru haki yangu imepatikana sasa ingawa kwa kuchelewa ila niliamini kuwa watalipa tu maana kulikuwa hakuna namna, wao ndio walivunja mkataba pasipo kufuata taratibu nami nilifuata taratibu za kudai haki yangu,"  alisema Mosoti.

Mosoti alifungua kesi hiyo mwaka juzi kupitia mwanasheria wake ambapo alishinda kesi hiyo lakini Simba hawakuweza kumlipa kwa kipindi walichokuwa wameagizwa na hivyo kusababisha deni hilo kuongezeka zaidi.

Post a Comment

 
Top