BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
SIKU moja baada ya Serikali kupitia Wizara ya Habari Sanaa Utamaduni na Michezo kusitisha kuchezwa kwenye vyombo vya habari mziki na video ya Chura, leo msanii Snura Mushi amejitokeza hadharani kuomba radhi kutokana na kadhia hiyo.

Meneja wa msanii huyo Hemedi Kavu maarufu kama HK alisema wamejitokeza hadharani kuomba radhi kutokana na video ya wimbo huo kukosa maadili na kudhalilisha utu wa mwanamke huku akikiri ni kweli haifai kutazamwa.

"Tunakiri tumekosea na sisi ni waungwana ndiyo maana tumekuja kwenu leo hii, tunaahidi haitojirudia tena na wasanii wengine wajifunze kupitia sisi" alisema HK.

Kwa upande wake msanii Snura alisema taarifa zilipotoshwa za kuwa wimbo wake ulifungiwa ukweli ni kwamba video ilisitishwa mpaka irekebishwe ndiyo itaruhusiwa na tayari wameanza kuifanyia marekebisho ili ianze kurushwa hewani.

"Mimi sikufungiwa na wimbo wangu pia ili nilisitishwa kufanya maonesho kutokana na kukosa kibali toka Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA)" alisema Snura.

Aidha Meneja wa msanii huyo alisema tayari Snura kashajisajili BASATA na kuanzia sasa anaruhusiwa kufanya maonesho mahali popote huku wimbo wa chura ukiwa ndiyo unasubiri marekebisho ambayo yatafanyika muda mfupi kutoka sasa.

Post a Comment

 
Top