BOIPLUS SPORTS BLOG

✏Sheila Ally, Dar
WANACHAMA wa klabu ya Acacia Stand United ya mjini Shinyanga leo Jumamosi jioni wameteua kamati ya watu watano ambao wataongoza klabu hiyo mpaka uchaguzi utakapofanyika mwezi Julai.

Mwenyekiti wa muda wa klabu hiyo ni Soud Rashid ambaye atashika nafasi ya Aman Vicent wakati Katibu mkuu aliyeteuliwa ni Kenedy Nyange huku wajumbe wakiwa ni Jacqline Isaro, Abdul Makusudi na Richard Luhende.

Mkutano huo wa wanachama na wadau wa Stand United umefanyika katika Uwanja wa CCM Kambarage ikiwa ni amri ya Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye ukisimamiwa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga mjini, Josephine Mtiro anayekaimu pia nafasi ya Mkuu wa Mkoa.

Hivi karibuni aliyekuwa Mwenyekiti wa Stand, Aman aliitisha mkutano uliohudhuliwa na wanachama 52 uliokuwa na lengo la kufanya mabadiliko ili klabu hiyo iwe Kampuni jambo ambalo limepingwa vikali na wanachama waliohudhuria mkutano wa leo na kwamba wanataka Stand United ibaki kuwa klabu.

Wanachama hao walipeleka malalamiko yao katika vyombo husika vya michezo ikiwemo kumwandikia barua Nape ambaye alitoa amri hiyo ya kuitisha mkutano ili wanachama ndiyo wachague kati ya kuwa Kampuni au kubaki klabu.

Viongozi walioteuliwa wamepewa majukumu matatu ambayo ni kuendelea kuandikisha wanachama, kusimamia shuguli za uchaguzi pamoja na kufanya kazi zote za klabu.

Imeelezwa kuwa wanachama hao pia walihoji uuzwaji wa gari la timu hiyo pamoja na mapato na matumizi zikiwemo fedha za wadhamini huku wakipendekeza uongozi ulioondolewa madarakani ufanyiwe uchunguzi.

Post a Comment

 
Top