BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally

STRAIKA wa Yanga, Amissi Tambwe juzi Jumanne alifikisha mabao 20 na kujikita kileleni kwa upachikaji wa mabao akimzidi Hamisi Kiiza wa Simba na kutamka kwamba anaamini atafunga sana ila hana haraka na mabao hayo.


Kiiza yeye amefikisha mabao 19 ingawa pia kasi yake imepungua na hiyo huenda inatokana na timu yake kufanya vibaya katika mechi tatu mfululizo ikiwemo ile ya Kombe la FA waliyopoteza dhidi ya Coastal Union.


Ni muda kidogo umepita bila straika huyo raia wa Burundi kupachika mabao hali ambayo ilipelekea mashabiki waanze kusema kwamba kiwango chake kimeshuka ila yeye aliiambia BOIPLUS kuwa katika timu si lazima afunge yeye bali kazi yake pia inamruhusu kumtengenezea mwingine nafasi ya kufunga.


Tambwe alisema kuwa anasikia kila jambo linalozungumzwa juu yake ila mashabiki watambue kuwa mchezaji yoyote anayeingia uwanjani ana nafasi ya kufunga ama kutoa mchango kwa timu ili ipate matokeo mazuri kazi ambayo pia anaifanya.


''Nashukuru Mungu nimefikisha idadi hiyo ya mabao, mechi bado zipo nyingi hivyo siwezi kujithibitishia moja kwa moja kuwa nitakuwa mfungaji bora au lah. Najua nafukuzana na Kiiza hivyo lolote linaweza kutokea maana mechi zimebaki nyingi.


''Kikubwa napenda kuona timu yangu inapata matokeo mazuri haya mambo ya ufungaji bora ni mipango ya Mungu, ila watu watambue kwamba kazi ya uwanjani si yangu peke yangu na si kila mechi nifunge mimi bali naweza kumsaidia mwingine afunge,'' alisema Tambwe.

Post a Comment

 
Top