BOIPLUS SPORTS BLOG

✏Waandishi Wetu
TIMU tatu za jiji la Tanga zimeshuka daraja rasmi leo na hivyo wakazi wa Jiji hilo hawatashuhudia tena mechi za Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Katika mechi za mwisho za kufunga pazia la VPL, Mgambo wala African Sports ambazo angalau zilikuwa zinapambana kushinda mechi zao za leo lakini wameshindwa baada ya wapinzani wao kuwakalia kooni huku Coastal wenyewe tayari walitangulia kushuka daraja.

Azam wamefanikiwa kumaliza ligi kwa kushika nafasi ya pili wakifikisha pointi 64 baada ya kulazimisha sare na Mgambo ya bao 1-1. Bao la Azam lilifungwa na Ramadhan Singano dakika ya 61 wakati Mgambo walipata penalti iliyofungwa na Chande Magoja dakika ya 72.

Mtibwa Sugar ikiwa nyumbani Uwanja wa Manungu iliifungashia virago African Sports kwa bao 2-0. Mabao ya Mtibwa yalifungwa na Hussein Javu na Jaffary Kibaya.

Simba ambao walikuwa wenyeji wa JKT Ruvu wameambilia kichapo cha mabao 2-1 mechi hiyo imechezwa Uwanja wa Taifa. Mabao mawili ya JKT yote yamefungwa na Abdulrahman Musa dakika ya kwanza na ya 30 huku Musa Mgosi akiifungia Simba bao pekee dakika ya 70.

Mabingwa wa VPL, Yanga wao wamelazimisha sare ya bao 2-2 dhidi ya  Majimaji kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea. Mabao ya Yanga yalifungwa na Paul Nonga dakika ya 15 huku Ally Mustafa 'Barthez' akisawazisha bao la pili kwa penalti dakika ya 90. Mabao ya Majimaji yalifungwa na Alex Kondo dakika ya 22 pamoja na Said Mrisho dakika ya 83.

Prisons imemaliza ligi ikiwa nafasi ya nne baada ya kuifunga Prisons bao 2-0 katiki mechi iliyochezwa uwanja wa Mkwakwani.Mabao ya Prisons yote yalifungwa na Jeremiah Juma aliyefikisha mabao 16.

Mbeya City yenyewe imetoka sare tasa na Ndanda mechi hiyo imechezwa uwanja wa Sokione jijini Mbeya wakati Stand United wakipata ushindi wa ugenini wa bao 1-0 dhidi ya Toto Africans ya jijini Mwanza bao la Stand limefungwa na Hassan Banda huku Kagera Sugar ikiifunga Mwadui bao 2-1.

Hivyo basi African Sports, Coastal Union na Mgambo JKT zimeshuka daraja ambapo nafasi zao msimu ujao zitachukuliwa na African Lyon, Mbao pamoja na Ruvu Shooting.

Yanga ndiyo mabingwa na walikabidhiwa kombe lao Azam wanashika nafasi ya pili, Simba wanabaki nafasi ya tatu, Prisons wapo nafasi ya nne huku Mtibwa Sugar wakishika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi.

Post a Comment

 
Top