BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
UKIZUNGUMZIA mabeki wasumbufu wa Ligi Kuu Bara basi huwezi kuacha kulitaja jina la beki wa kushoto wa Simba, Mohamed Hussein 'Tshabalala'.

Tshabalala ni beki mwenye kasi, anakaba na anaweza pia kupiga mipira wa krosi, ni beki ambaye anategemewa kwenye kikosi hicho.

Tshabalala ni matunda ya Friends Rangers yenye maskani yake Magomeni Kagera ingawa Simba walimsajili beki huyo akitokea Kagera Sugar.

BOIPLUS ilifanya mahojiano maalumu na mchezaji huyo akiwa nyumbani kwake Magomeni Kagera ambapo alielezea mambo mbalimbali kuhusu soka lake ikiwemo mwenendo mbaya wa timu yake kwenye michuano ya ligi;

SIMBA KUSHINDWA KUCHUKUA UBINGWA
Simba haijachukuwa ubingwa kwa misimu minne sasa ingawa msimu huu ilikuwa na uwezo mkubwa wa kuchukua ubingwa kutokana na jinsi ilivyokuwa ikifanya vizuri kutokana na wachezaji kuwa na morali kubwa.


''Wachezaji tulikuwa na morali lakini kilichotokea ni tofauti na matarajio yetu, mashabiki wetu waliumia kadhalika na sisi ila tunajipanga msimu ujao ili tufanye vizuri zaidi,'' alisema Tshabalala

NINI KIBORESHWE
''Kwa maoni yangu Simba inahitaji mshambuliaji mwenye uwezo wa kuifungia magoli mawili na zaidi katika kila mchezo kwa kuwa safu nyingine ndani ziko vizuri,''

SOKA LA KULIPWA
Tshabalala alisema ana ndoto za kucheza soka nje ya nchi kabla hajajiunga na Simba kutokea Kagera Sugar, na ligi ya Afrika Kusini ndiyo anayoipenda zaidi.

''Kama Mungu atajalia nitakwenda Afrika Kusini kucheza soka basi  ningependa kuchezea Kaizer Chief ndiyo timu ninayoipenda na ninaamini itanipa mafanikio makubwa,'' alisema

AJIB NDIYE JEMBE
Tshabalala alimtaja Ibrahim Ajib kuwa ndiye mchezaji anayemkubali kuliko wote ndani ya Simba na kusema:  ''Mshambuliaji huyo ni mdogo kiumri na  ana kipaji, huwa nafarijika akiwepo uwanjani wakati wa mechi,''

MAKOCHA WAZUNGU vs WAZAWA
Tshabalala alisema amewahi kuwa chini ya makocha mbalimbali wa ndani na nje ya nchi katika timu ya Simba lakini amewataja makocha wa kigeni kuwa wepesi wa kuwaelewa wachezaji.

''Wazungu huwa wanatuelewa haraka  na wanatusoma saikolojia zetu haraka pia kuliko wazawa kwakuwa kila wanaloelezwa wanahisi wanadanganywa,''  alisema Tshabalala

MCHEZAJI BORA VPL
Kila mtu anapenda kuwa namba moja kwa kila jambo ndiyo maana hata Tshabalala ameweka wazi kuwa yeye ndiye Mchezaji Bora wa msimu huu.

''Ukiniambia nimtaje mchezaji bora wa ligi msimu huu ni mimi na anayenifuatia ni Juma Abdul wa Yanga, tumekuwa katika kiwango bora sana msimu na tuna stahili,''

ATAMANI NYOTA YA MARCELO
Tshabalala alisema anavutiwa na soka la mchezaji wa Real Madrid raia wa Brazil, Marcelo na anaimani siku moja atafikia kiwango chake ingawa Jabir Aziz wa Mwadui FC ndiye mchezaji  anayemvutia katika soka la Bongo.

BABA UBAYA ALIMVURUGA
Beki huyo wakati anajiunga na Simba msimu wa 2014/15 Kutokea Kagera Sugar alimkuta beki Issa Rashidi 'Baba Ubaya' akiwa kwenye ubora wake hivyo ushindani wa namba ulimfanya Tshabalala aongeze juhudu.

''Haikuwa kazi rahisi kumkalisha benchi Baba Ubaya na kupata namba, nilifanya mazoezi kwa bidii ili nifanikishe lengo langu kwani Baba Ubaya ni mchezaji mzuri,'' alisema Tshabalala

JEZI NAMBA 15
Tangu atue Simba jezi namba yake ni 15, hajawahi kubadilisha na ameweka wazi kuwa haina maana yoyite na hata akipata nyingine ataweza kuivaa ila kwa wakati huo anatu Simba aliikuta hiyo.

NJE YA SOKA
Tshabalala hana mke wala mtoto ila ana mchumba ambaye amemwelezea kuwa ana msaada mkubwa kwake katika kumshauri mambo mbalimbali na anapokuwa nyumbani anapenda kusikiliza muziki, kuangalia filamu za aina zote, pia huvutiwa zaidi na muigizaji Jimmy Mafufu pamoja na msanii wa nyimbo za kizazi kipya maarufu kama Bongo Flava, Mirror.

Post a Comment

 
Top