BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Mbeya
WACHEZAJI wawili wa timu ya Yanga Mbuyu Twite na Vincent Bossou watafanyiwa vipimo zaidi leo jijini Dar es Salaam baada ya kupata maumivu katika mchezo dhidi ya Mbeya city uliopigwa kwenye uwanja wa Sokoine.

Twite alitolewa dakika ya tatu baada ya kugongwa kwenye ugoko na kiungo Ramadhani Chombo 'Redondo' huku Bossou akiumizwa puani na Hassan Mwasapili.

Daktari wa timu hiyo Edward Bavu alisema watawafanyia vipimo zaidi leo ili kujua ukubwa wa tatizo ila kuna uwezekano wakawa wameumia sana.

"Bossou ameumizwa puani na Twite mguuni tunaenda kuwafanyia vipimo zaidi ili kufahamu ukubwa wa tatizo ila wanaonekana wameumia sana," alisema Bavu.

Licha ya kuwa ligi inaelekea ukingoni lakini mchango wa wachezaji hao kwa timu ni mkubwa hasa  Bosou ambaye amekuwa mhimili mkubwa katika safu ya ulinzi baada ya nahodha Nadir Haroub kuwa majeruhi kwa muda mrefu.

Yanga wametawazwa kuwa mabingwa wa ligi kuu msimu wa 2015/16 lakini wana michezo miwili mikubwa dhidi ya Sagrada Esparanca ya Angola Mei 17 kombe la shirikisho na fainali ya kombe la FA June 11 watakaocheza na Azam Fc.

Post a Comment

 
Top