BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Dar
IKIWA ni saa chache tangu 'maproo' wa Simba kugoma kuondoka na wenzao kwenda Songea wakidai walipwe mishahara yao kwanza, hatimaye viongozi wa timu hiyo wamewalipa mishahara hiyo mchana wa leo.

Kikosi cha Simba chenye wachezaji 13 wakiwemo wa kikosi cha vijana sasa wamefika mjini Songea tayari kwa mechi yao ya keshokutwa dhidi ya Majimaji. Timu hiyo iliondoka saa 11 alfajiri ya leo.

Nyota hao wa kigeni ambao ni Hamisi Kiiza, Vincent Angban, Juuko Murshid, Justice Majabvi, Emiry Nimubona, Brian Majwega pamoja na Raphael Kiongera waliitwa mchana ofisi kwa Rais wa Simba, Evans Aveva ambako walijieleza pamoja na kulipwa mishahara yao.

Habari kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa viongozi wa Simba wanafikiria kuwasafirisha wachezaji wao wawili tu Majabvi na Angban kwenda kuongeza nguvu na kama watawasafirisha basi watatakiwa kesho Jumanne ndio waanze safari hiyo.

Wachezaji hao walizungumza na BOIPLUS mara baada ya kutoka kwenye kikao chao cha pamoja na baadhi ya viongozi wao, walisema kuwa hawakutendewa haki ndio maana walikubaliana kwa pamoja kutoondoka.

''Tumelipwa tayari mishahara yetu ila Majabvi na Angban wanaweza kwenda huko kesho kama viongozi watakuwa hawajabadilisha mawazo yao maana walikuwa wanafanya mpango wa kuwasafirisha, kuna mgawanyiko mle ndani wengine hatutakiwi hivyo tunasubiri ligi iishie ili tumalizane,'' alisema mchezaji huyo kwa sharti la kutoandikwa jina lake mtandaoni.

Post a Comment

 
Top