BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu
WANACHAMA wa Klabu ya Simba wilaya ya Temeke wameutaka uongozi wa klabu hiyo kuimarisha kikosi chao cha msimu ujao kwa kusajili wachezaji mahiri wakitumia fedha za malipo ya mshambuliaji wao wa zamani Emmanuel Okwi.

Hivi karibuni uongozi wa timu ya Etoile  du Sahel ya Tunisia iliilipa Simba zaidi ya dola 300,000 ambazo zilikuwa deni la mauzo ya Okwi.

Wanachama hao ambao pia walimweleza Rais wa Simba, Evans Aveva katika mkutano wao wa wanachama wa matawi yote ya Simba Wilaya Temeke kuhakikisha kikosi cha msimu ujao kinakuwa na ushindani mkubwa kwa kusajili wachezaji bora na wapambanaji.

Mwenyekiti wa matawi hayo, Fortunatus John alisema kuwa kwa sasa Simba inakabiliwa na changamoto kama kutokuwa na Katibu Mkuu, Jengo la klabu limekodishwa pamoja na kuwepo kwa migogoro baina ya wachezaji na viongozi jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya klabu yao.

''Timu yetu haina ushindani, kikubwa tunachoomba ni usajili wa maana msimu ujao na fedha za mauzo ya Okwi zitumike kusajili wachezaji wazuri badala ya kujenga uwanja wa Bunju,'' alisema.

Akijibu maoni na maswali ya wanachama Aveva alisema kuwa: ''Tulipoingia madarakani tulikabidhiwa timu ikiwa nafasi ya nne na sio ubingwa, tunaamini hapa tulipofika tunasogea ila tutaimarisha zaidi kikosi chetu msimu ujao.''

Post a Comment

 
Top