BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Zainabu Rajabu, Dar
KOCHA wa Simba, Jackson Mayanja jana Jumapili aliuangalia mchezo wa timu yake ilipocheza na Azam FC na kutamka kwamba washambuliaji wake walipoteza umakini ndiyo maana walishindwa kufunga.

Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam timu hizo zilitoka sare tasa na kuifanya Simba iendelee kubaki kwenye nafasi yake ya tatu ikiwa na pointi 58.

Simba walitengeneza nafasi nyingi kipindi cha kwanza lakini safu iliyokuwa chini ya Hamisi Kiiza mwenye mabao 19 ilishindwa kupenya ngome ya Azam.

Mayanja alikuwa jukwaani akitumikia adhabu yake aliyopewa wakati wa mechi yao na Toto Africans iliyochezwa uwanjani hapo na kuambulia kipigo cha bao 1-0 huku akieleza kuwa kikosi chake kilikuwa na uwezo wa kumaliza mchezo kipindi cha kwanza.

"Washambuliaji wangu hawakuwa makini kwani walipata nafasi ila hawakuzitumia, tulikuwa na uwezo wa kumaliza mechi kipindi cha kwanza,'' alisema Mayanja.

Kocha huyo raia wa Uganda alichukua mikoba ya Muingereza, Dylan Kerr aliyetupiwa virago na kuingoza timu hiyo kushinda mechi nane za kwanza ikiwa chini yake.

Post a Comment

 
Top