BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Mwandishi Wetu, Mbeya
KIKOSI cha Yanga kimefanya mazoezi yake ya mwisho katika uwanja wa Sokoine kwa ajili ya mchezo wao wa ligi kuu Vodacom unaopigwa kesho dhidi ya Mbeya City.

Yanga wamewasili  asubuhi ya leo kwa usafiri wa ndege baada ya kuwapa wachezaji wake 
mapumziko ya siku mbili tangu walipomaliza mechi yao ya kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya GD Sagrada Esperanca ya Angola.

Akizungumza na BOIPLUS  baada ya kuwasili mkoani humo, Meneja wa timu ya Yanga, Hafidh Salehe alisema kuwa wachezaji wote wapo salama isipokuwa kuna baadhi yao hawajaambatana na timu.

Hafidh amesema, wameenda na kikosi cha wachezaji 21 tu huku Malimi Busungu , 
Issoffou Obubacar ambao wote ni majeruhi pamoja na Benedict Tinoco wamesalia Jijini  Dar es salaam.

"Wachezaji watatu wamebaki akiwemo Busungu na Issoffou ambao wote ni majeruhi ila 
Tinoco amebaki kwani tuliamua kuondoka na makipa wawili tu,"alisema Hafidh.

Meneja huyo aliongeza kuwa hawatadharau mchezo wowote kwani wanataka kuhakikisha wanashinda kila mechi inayokuja mbele yao na huo ndio mkakati wao toka kuanza kwa ligi.

"kwetu kila mchezo ni fainali na tunataka kushinda michezo yote iliyosalia na kuonyesha 
kuwa ubingwa hatujauapata kwa kubebwa kama inavyosemwa, wachezaji wote wamejiandaa kushinda michezo yote iliyosalia."

Yanga wenye alama 68 wakisalia na michezo mitatu mkononi wameweza kutwaa ubingwa huo baada ya timu za Azam na Simba kutoweza kufikia alama hizo hata kama watashinda michezo yao yote iliyobaki.

Naye Mwenyekiti wa Mbeya City Mussa Mapunda amesema kuwa ana imani kikosi chao kitapata ushindi kwenye mchezo wa kesho dhidi ya Yanga hasa baada ya kuimarika kwa wachezaji wake.

Mapunda amesema kuwa, hawatakubali kufungwa kwa mchezo huo kwani una umuhimu sana kwao ili kuweza kusonga katika nafasi za juu

Mbeya City wamekuwa na rekodi mbaya pale wanapokutana na Yanga na kushindwa kufurukuta hata wakiwa katika uwanja wao wa nyumbani.

Post a Comment

 
Top