BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Shinyanga
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga wameendeleza ushindi baada ya kuifunga Stand United bao 3-1 kayika mechi iliyochezwa Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga na kuifanya Yanga ifikishe pointi 68.

Hii ni mechi ya pili kwa Yanga kushinda Kanda ya Ziwa ambapo mechi iliyopita waliifunga Toto Africans bao 2-1, mechi iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini na Mwanza.

Donald Ngoma aliipatia Yanga mabao mawili katika kipindi cha kwanza ambayo yote alifunga kwa kupiga mashuti yaliyomshinda kipa wa Stand United Frank Muwonge, bao la kwanza alifunga dakika ya pili na lingine alilifunga dakika ya 44.

Dakika ya 23, Salum Telela alikosa bao baada ya shuti lake kutoka nje kidogo ya goli huku Elius Maguli akijibu mapigo dakika ya 30 akipangua ngome ya Yanga iliyoongozwa na Nadir Haroub 'Canavaro' na Kelvin Yondan lakini umakini wa Deogratius Munishi 'Dida' uliweza kuokoa hatari hiyo.

Kipindi cha pili kilipoanza kocha wa Yanga, Hans Pluijm alifanya mabadiliko ambapo aliwatoa Telela, Kelvin Yondani na Ngoma waliingia Mbuyu Twite, Vincent Bossou pamoja na Matheo Anthony.

Kocha wa Stand United, Patrick Liewig naye aliwatoa Salum Kamana, Vitalis Mayanga na kuwaingiza Pastory Athanas na Frank Hamis.

Mwamuzi wa mchezo huo Emmanuel Mwandembwa alitoa kadi ya njano kwa Jacob Masawe aliyemchezea rafu Simon Msuva na kipa wa Yanga, Dida kwa kuchelewa kupiga mpira.

Amissi Tambwe ambaye idadi yake kubwa ya mabao katika msimu mmoja ilikuwa ni 19, aliifungia bao la tatu Yanga na yeye kuvunja rekodi yake kwa kufikisha mabao 20 akipokea mpira wa kona iliyochongwa na Msuva ikiwa ni dakika ya 63 huku Elius Maguli akiifungia timu yake bao la kufutia machozi kwa mkwaju wa penalti dakika ya 82 baada ya Pastory kuchezewa rafu eneo la hatari.

Yanga inajiandaa kucheza na Mbeya City ambapo pia itakuwa ugenini Mei 10 wakati Stand United wataikaribisha Coastal Union.

Post a Comment

 
Top