BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
TIMU ya Yanga imepiga hatua moja mbele katika kombe la shirikisho barani Afrika baada ya kuifunga G.D Sagrada Esparanca ya Angola kwa goli 2-0 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Yanga walianza mpira kwa kasi na dakika ya kwanza beki Juma Abdul alipiga shuti kali langoni mwa Sagrada lakini mlinda mlango Roadro Juan Sesemero alikuwa makini na kuondoa hatari hiyo iliyozaa kona.

Yanga waliendelea kumiliki mpira na kushambulia lakini mabeki wa Sagrada walikuwa makini sana huku wakipoozesha mchezo kwa kujiangusha ili kupunguza mashambulizi ya wanajangwani. 

Kipindi cha pili Yanga walifanya mabadiliko ya kumtoa Salum Telela na kumuingiza Mbuyu Twite ambaye aliongeza nguvu katika eneo la kiungo  kwa kukaba, kupandisha timu kwa haraka na kupiga mipira mirefu kwa mawinga.

Dakika ya 72 Simon Msuva aliipatia Yanga goli la kwanza baada ya kumalizia krosi safi ya Geofrey  Mwashiuya aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Malimi Busungu ambaye alitolewa kwa machela baada ya kugongana na mlinda mlango wa Sagrada,Tavazes.

Yanga waliendelea kulisakama lango la Sagrada na dakika ya 90 Matheo Anthony aliipatia Yanga goli la pili kwa shuti kali nje ya kisanduku cha penati.

Ushindi huo ni mzuri kwa Yanga hasa kwavile wamewazuia wageni kupata bao, hata hivyo Sagrada wamecheza vema hivyo kuashiria mchezo wa marejeano utakuwa mgumu.

Post a Comment

 
Top