BOIPLUS SPORTS BLOG

✏Bakari Kagoma, Dar
SHIRIKISHO la mpira wa miguu Tanzania TFF, limetangaza kutoandaa michuano ya Kagame iliyopangwa ifanyike jijini Dar es Salaam mwezi ujao kutokana na kubanwa na ratiba ya mechi za kimataifa.

Awali michuano hiyo ilitakiwa ifanyike visiwani Zanzibar lakini walijitoa katika hatua za mwisho kutokana na mipango yao kutokwenda sawa na kurudisha mpira Tanzania bara.

Akizungumza na BOIPLUS, Ofisa habari wa shirikisho hilo Alfred Lucas alisema wamefikia hatua hiyo kutokana na ratiba ya mechi za kimataifa ya timu ya Taifa na klabu ya Yanga ambao wameingia katika hatua ya makundi ya kombe la shirikisho barani Afrika hivyo wakiwa waandaji watashindwa kuwahudumia ipasavyo wageni wataokuja.

" Ni rasmi kwamba hatutaandaa michuano ya kombe la Kagame kutokana na muingiliano wa ratiba ya michuano hiyo na mechi za kimataifa za klabu ya Yanga na timu ya Taifa hivyo itakuwa ngumu kwetu, tumewaandikia barua CECAFA kuwajulisha juu ya hilo," alisema Alfred.

Baraza la michezo la ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na kati CECAFA limekuwa likiitumia Tanzania kuandaa michuano hiyo endapo kuna mwanachama atashindwa kufanya hivyo na wamekuwa wakifanikiwa kutokana na kuwepo kwa mashabiki wengi wanaopenda soka.

Mwaka jana michuano hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam ambapo timu ya Azam ilitawazwa kuwa mabingwa kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo.

Post a Comment

 
Top