BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Akram Msangi, Dar
SIKU moja baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kurudisha nyuma mchezo wa fainali ya Kombe la FA uliopangwa kufanyika Mei 25, Uongozi wa Yanga umelitaka shirikisho hilo kusogeza mechi hiyo mbele kwani ratiba imewabana.

Awali fainali hiyo ilikuwa ifanyike Juni 11 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam lakini jana Jumatano TFF ilitangaza mabadiliko ya ratiba hiyo na kuirudisha nyuma hadi Mei 25.

Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Jerry Muro alisema kuwa timu yake haijawahi kupumzika na itarejea kesho mchana na kuingia kambini tayari kwa mechi yao ya mwisho dhidi ya Majimaji itakayochezwa Mei 22, mjini Songea ambapo watatakiwa kucheza fainali hiyo na Azam FC siku tatu baada ya kumalizika ligi.

"Timu inaingia kesho toka Angola, keshokutwa tunasafiri kwa basi kuelekea Songea, tukirudi baada ya siku mbili tunatakiwa tucheze fainali na Azam, kweli hata hao wachezaji wetu si wanachoka," alihoji Muro.

Muro ameitaka Serikali kuingilia kati na kuona kama wanaweza kuwasaidia mabingwa hao katika suala hilo kwakuwa timu hiyo inawakilisha nchi katika michuano ya kimataifa ili izidi kupeperusha bendera ya Taifa.

Post a Comment

 
Top