BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Mwanza
YANGA hawataki kulala. Jana wameipiga Toto Africans ya jijini Mwanza bao 2-1 na leo mapema wametua mjini Shinyanga kwa ajili ya mechi yao na Stand United itakayochezwa keshokutwa Jumanne kwenye Uwanja wa CCM Kambarage.

Kuwahi kwa Yanga ni kutaka kuwapa wachezaji muda wa kupumzika ili kuwa imara kwenye mechi hiyo ambayo wanataka washinde na kujikita zaidi kileleni mwa ligi kwani sasa wamekusanya pointi 65  huku wakibaki na mechi nne mkononi.

Mechi yao ya jana iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ilizua tafrani kwa upande wa baadhi ya wanachama wa Toto wenye msimamo mkali ambao waliwashukia baadhi ya viongozi wa timu hiyo wakidai kuwa kukaa kwao pembeni wakati wa mechi hiyo ndiko kulichangia kupata kipigo hicho.

Habari ambazo zilizagaa uwanjani hapo ni kwamba baadhi ya viongozi na wachezaji walituhumiwa kuhujumu timu yao kwa mapenzi waliyonayo dhidi ya Yanga.

BOIPLUS ilishuhudia gari lililokuwa limewabeba wachezaji wa Toto likitoka uwanjani hapo huku wachezaji wakilumbana kwa maneno makali na wakitupiana lawama kuwa wamepoteza mechi kwa uzembe wao na si kwamba walizidiwa na Yanga.

Kiungo wa Toto, Abdallah Seseme alisema kuwa ''Inaumiza sana hii ilikuwa ni mechi ya kupatia pesa endapo tungeshinda lakini imekuwa tofauti na unadhani nani atatoa pesa katika mechi zilizobaki hata tukishinda.

''Leo hii tungewafunga Yanga tungepata pesa nyingi ndiyo maana wachezaji wamekasirika. Kuhusu hizo tuhuma hakuna mwenye uhakika nazo na malumbano ya viongozi yaliyotokea hayo ni mambo yao wenyewe. Sisi tunasubiri kikao kwani walisema watakuja kujadili na sisi muda wowote tu,'' alisema Seseme.

Toto wanajiandaa na mechi ya ugenini dhidi ya Prisons itakayochezwa jijini Mbeya. Yanga wao watacheza na Stand ambao wamepoteza mchezo uliopita dhidi ya Mwadui.

Post a Comment

 
Top