BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Akram Msangi, Dar
LICHA ya kuwa dirisha la usajili halijafunguliwa, vigogo wa soka nchini,  Simba na Yanga wameanza kupigana vikumbo mtaani kusaka wachezaji wa kuimarisha vikosi vyao msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

BOIPLUS ilishuhudia filamu moja ambayo 'Sterling' wake alikuwa kiungo wa Coastal Union, Juma Mahadhi huku vigogo wa Simba na Yanga wakichuana kumuweka mkononi kinda huyo aliyewahi kuwadhuru watoto wa Jangwani kwenye mchezo wa ligi  uliochezwa jijini Tanga.

Mchezo ulianza juzi kwa vigogo wa Yanga kumtumia nauli Mahadhi ili atue jijini Dar es Salaam wakae mezani kuweka mambo sawa lakini wakati kiungo huyo yuko njiani jana, alipokea 'mkwanja' kwenye simu yake ambao ulitoka kwa kiongozi wa Simba ambao alielezwa kuwa ni nauli.

Baada ya Mahadhi kufika Ubungo alipokelewa na watu wa Yanga waliompeleka moja kwa moja hadi makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo kwenye makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani ambapo BOIPLUS inafahamu kuwa wameshafanya makubaliano ya awali.

Wakati Mahadhi yuko Jangwani, alipigiwa simu na kiongozi mmoja wa benchi la ufundi la Simba (jina tunalo) akimuuliza mahali alipo lakini Mahadhi alishindwa kutoa ushirikiano kwavile waliomfanya aje Dar es Salaam ni Yanga na kwamba licha ya kuwa Simba ndio walikuwa wa kwanza kuzungumza naye ila  walikuwa wa mwisho kutuma nauli.

Mtandao huu ulimtafuta Mahadhi usiku wa jana ili kujua mahali alipo ndipo kiungo huyo aliposema kuwa amerejea jijini Tanga huku akikiri kuwa Yanga wamefuata njia sahihi kwa kuwasiliana na Meneja wake Khalid Abdallah tofauti na Simba ambao walikuwa wakizungumza na yeye pekee.

Mahadhi hajasaini mkataba rasmi wa kuitumikia Yanga msimu ujao kwavile dirisha la usajili bado halijafunguliwa, hivyo ni wazi kuwa kilichofanyika kati  ya pande hizo mbili ni kusaini makubaliano ya awali tu na hakuna malipo yoyote yaliyofanyika.

Imeelezwa kuwa Yanga wapo tayari kumpa Sh 30 milioni kwa miaka miwili wakati Simba ilitaka kumpa Sh 15 milioni kwa miaka mitatu.

Post a Comment

 
Top