BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
MABINGWA wapya wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara timu ya Yanga imepata mapokezi ya kifalme katika uwanja wa ndege wa mwalimu Julius Nyerere walipokuwa wanarejea toka Angola walikofuzu hatua ya makundi ya kombe la shirikisho barani Afrika.

Yanga imefuzu hatua hiyo licha ya kukubali kichapo cha goli 1-0 toka kwa Sagrada Esparanca ya Angola baada ya kuifunga magoli 2-0 katika mchezo wa awali uliopigwa katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam wiki moja na nusu iliyopita.

Mkuu wa kitengo cha Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Jerry Muro aliwashukuru wapenzi na wanachama wa klabu hiyo kwa kujitokeza kwa wingi kuwalaki mashujaa wao waliofuzu hatua hiyo kw mara ya kwanza tangu mwaka 1998 hatua ya makundi ya klabu bingwa Afrika.

"Tunawashukuru sana wapenzi wetu kwa kujitokeza kwa wingi na imeonyesha sisi ni wakimataifa, kuanzia benchi la ufundi, wachezaji uongozi hadi mashabiki," alisema Jerry.

Katika hali isiyo ya kawaida mashabiki walikuwa ni wengi mpaka ikatishia usalama wao kitu kilichopelekea Polisi kufanya kazi ya ziada kuwatuliza mashabiki hao waliolipuka kwa shangwe.

Aidha Msemaji wa klabu hiyo alitumia ushawishi wake ndani ya timu kuwatuliza mashabiki waliofurika uwanjani hapo hasa wachezaji walipokuwa wanatoka nje.

Post a Comment

 
Top