BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Mbeya
TIMU ya Yanga imejihakikishia ubingwa wa asilimia mia moja baada ya kuibuka na ushindi  wa magoli 2-0 dhidi ya Mbeya city kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania bara uliofanyika katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Mabingwa hao walipata pigo dakika ya tatu baada ya kiungo wake Mbuyu Twite kutolewa nje kwa kuumizwa na Ramadhani Chombo na nafasi yake kuchukuliwa na Salum Telela.

Vincent Bossou aliipatia bao la kwanza Yanga dakika ya 15 baada ya kupokea mpira wa krosi uliopigwa na Juma Abdul kutokana na kona fupi ya Simon Msuva.

Dakika tisa baada ya goli hilo Bossou nae alitolewa nje baada ya kugongana na beki Hassani Mwasapili na mabingwa hao kulazimika kufanya mabadiliko ya wachezaji wawili ndani ya dakika 26 pekee.

Mashabiki wa Mbeya city walianza kurusha chupa na mawe uwanjani baada ya kutokubaliana na mwamuzi baada ya mshambuliaji Donald Ngoma kuonekana amejiangusha na refa kuonesha faulo kuelekea upande wa wenyeji.


Yanga walifanya shambulizi Kali langoni mwa Mbeya city ambapo Ngoma alimpiga chenga beki Haruna Shamte kisha kubaki na mlinda mlango Juma Kaseja lakini shuti lake liligonga mwamba na kutoka nje.

Hata hivyo Mbeya city watabidi wajilaumu wenyewe ambapo mshambuliaji wake Salvatory Nkulula akiwa amebaki na nyavu alishindwa kutumbukiza mpira kimiani baada ya kuanguka chini.

Huku wengi wakidhani matokeo yatabaki kuwa bao 1-0, mshambuliaji Hamisi Tambwe aliipatia Yanga goli la pili dakika ya 85 na kufikisha magoli 21 baada ya kuachia shuti kali nje ya kisanduku cha 18 na kumshinda mlinda mlango Kaseja.

Yanga ambayo imefikisha pointi 71 ilimtoa pia Deus Kaseke na nafasi yake ikachukuliwa na Godfrey Mwashiuya huku Mbeya city wakimtoa Joseph Mahundi na kumuingiza Ditram Nchimbi.

Post a Comment

 
Top