BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Akram Msangi, Dar
UONGOZI wa Klabu ya Yanga unajiandaa kupeleka barua ya malalamiko katika shirikisho la soka  barani Afrika (CAF) kutokana na kufanyiwa vitendo visivyo vya kimichezo timu yao kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya GD Sagrada Esparanca uliofanyika nchini Angola jana.

Katika mchezo huo mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara walikubali kipigo cha bao 1-0 na kufanikiwa kusonga mbele katika hatua ya makundi baada ya mchezo wa awali kushinda magoli 2-0 uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 2-1.

Moja ya vitendo vibaya ambavyo walifanyiwa Yanga ni kupigwa kwa kipa wao Deogratius Munishi Dida' na mashabiki wa wenyeji.

Msemaji wa Klabu hiyo, Jerry Muro alisema barua hiyo inaandaliwa na Katibu Mkuu wao na itatumwa CAF ili kuonesha kutoridhika kwao na matukio hayo na kulitaka shirikisho hilo kumfungia mwamuzi aliyechezesha mchezo huo baada ya kuvurunda katika mechi hiyo.

"Uongozi umesikitishwa na matukio hayo na hautayafumbia macho kutokana na kujirudia mara mara kwani hata katika mechi yetu dhidi Etoile du Sahel ya Tunisia tulifanyiwa vitendo hivyo," alisema Jerry.

Katika hatua nyingine kikosi cha mabingwa hao kitarejea kesho Ijumaa mchana kikitokea nchini Afrika Kusini na kitaenda moja kwa moja kambini kabla ya Jumamosi kusafiri kuelekea Songea kwa ajili ya mchezo  mwisho wa ligi dhidi ya Majimaji.

Muro aliwataka wanachama na wapenzi wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius M. Nyerere kuwapokea mashujaa wao.

Post a Comment

 
Top