BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar

KLABU ya African Lyon inayoshiriki ligi kuu Tanzania bara imeingia makubaliano na kituo cha Radio cha Choice FM kwa ajili ya kusaka vipaji vya wachezaji wa mpira wa miguu na kuwatangaza nje ya nchi ili iwe msaada mkubwa kwa Taifa.

Makubaliano hayo yataiwezesha Lyon yenye makao makuu yake Mbagala Dar es Salaam kuandaa mashindano na programu  ambazo zitahusisha vijana wa kike na wakiume.

Mkurugenzi mtendaji wa klabu hiyo Rahim Kangezi alisema makubaliano hayo yatawawezesha kupata wachezaji wazuri ambao watawatumia katika ligi kuu Tanzania bara na kuwauza ili kupata faida.

"Tunawashukuru wenzetu wa Choice FM kuingia makubaliano nasi ambayo yatatusaidia kupata wachezaji wazuri ambao tutaweza kuwauza nje ya nchi kama ilivyokuwa kwa Mbwana Samatta," alisema Kangezi.

Kwa upande wake mkuu wa vipindi wa Choice FM, Antonio Nugaz alisema kuwa kilichofanya kuingia makubaliano hayo ambayo ni ya miaka 10 ni kwamba  itasaidia kupata wachezaji ambao wataweza kuitangaza nchi kimataifa kama muziki wa Bongo fleva.

"Tanzania tumejaliwa kuwa na vipaji vingi vya soka lakini watu wengi hawajaviona, sisi na Lyon tumeamua kupita mtaa kwa mtaa kuvivumbua tukianzia Mbagala," alisema Nugaz.

Makubaliano hayo pia yalitumiwa kutangaza jezi mpya za klabu hiyo watakazo tumia msimu ujao wa ligi kuu Tanzania bara.

Post a Comment

 
Top